Famba: Picha ya maandamano Marekani yatumika kupotosha Corona

Rodgers George 0903Hrs   Juni 04, 2020 NuktaFakti
  • Ni habari inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikisema “Wamarekani hawana hofu tena na Corona”.
  • Habari hiyo siyo ya kweli kwani imetumia picha za Rais wa zamani wa nchi hiyo Barrack Obama alipokuwa kwenye maandamono mwaka 2015.

Dar es Salaam. Habari za uzushi hazina mipaka zinagusa kila eneo na kuathiri watu wa rika tofauti. Watu wenye nia ovu wanatumia picha za matukio yaliyopita kupotosha watu kuhusu ugonjwa wa virusi vya Corona. 

Huenda katika mtandao wa Facebook umekutana na picha ya maandamano yanayoongozwa na Rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama ikiwa na maandishi yanayosema “Wamarekani hawana hofu tena na Corona”

Picha hiyo haina mahusiano na janga la Corona linaloendelea sasa, licha ya kuwa ilitokea miaka ya nyuma katika matukio mengine huko Marekani.

Ukweli wa picha hiyo

Nukta Fakti imebaini kuwa picha hiyo ilipigwa Machi 8, 2015. Siku hiyo Obama na mke wake Michelle Obama waliungana na waandamanaji kuadhimisha miaka 50 tangu kupigwa kwa mwanaharakati wa haki za raia Amelia Robinson. 

Mwanaharakati huyo aliyekuwa kiongozi wa vuguvugu la haki za kiraia za Marekani katika mji wa Selma, Alabama alipigwa na polisi kutokana na ubaguzi wa rangi. 

Alifariki dunia Agosti 26 mwaka huo huo ambapo habari ya kifo chake  iliripotiwa kwenye tovuti ya Voice of America kwa kutumia picha hiyo.  


Zinazohusiana


Picha hiyo ni uzushi na haina ukweli wowote kuhusu Wamarekani kutokuogopa Corona. 

Kwa sasa Wamarekani katika baadhi ya majimbo wanaendelea na maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi baada ya kifo cha George Floyd, Mmarekani mweusi aliyekufa akiwa mikononi mwa polisi.

Related Post