CAG aibua madudu zaidi bodi ya mikopo elimu ya juu Tanzania

April 20, 2023 6:05 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Abaini mapungufu ya udhibiti wa taarifa za urejeshaji mikopo.
  • Programu muhimu hazikupewa kipaumbele utoaji mikopo. 

Dar es Salaam. Licha ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kushindwa kukusanya Sh611 bilioni za mikopo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameibaini bodi hiyo ina changamoto mbalimbali ikiwemo uthibiti wa taarifa za wanufaika wa mikopo.  

CAG Charles Kichere katika ripoti yake ya mashirika ya umma ya mwaka 2021/22 amesema hadi kufikia Juni 30, 2022, bodi hiyo ilikuwa na madai ya Sh611 bilioni ambayo yalikuwa yameiva lakini hayajakusanywa. 

“Mikopo iliyoiva haijakusanywa kutokana na kukosekana kwa ufanisi katika ukusanyaji na kutokuwepo kwa mfumo wa kushirikisha wadau muhimu,” amesema CAG Kichere katika ripoti hiyo.

Wadau hao ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi (NSSF). 

Suala hilo limeibua mjadala mpana kwenye jamii ambapo baadhi ya watu wamewataka wanufaika wa mikopo hiyo kurejesha fedha ili wengine wanufaike huku wengine wakishauri Serikali na wadau kufungua fursa za ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu kuwawezesha kupata kipato na hatimaye kurejesha fedha walizokopa. 

Wakati mjadala huo ukiendelea, CAG imeibua mambo mbalimbali ndani ya bodi hiyo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ikiwemo udhibiti wa taarifa za marejesho ya mikopo. 

“Mapitio ya mfumo fungamanishi wa usimamizi wa mikopo yalibaini upungufu katika udhibiti wa uhakiki wa malipo ya marejesho ya mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.


Zinazohusiana:


Amesema kukosekana kwa udhibiti wa kutosha wa uingizaji taarifa za marejesho ya mikopo kunaweza kusababisha kurekodiwa kwa marejesho yasiyokuwa na nambari za risiti za malipo katika mfumo. 

Hii inatokana na ukosefu wa udhibiti wa uhakiki wa kutosha katika mchakato wa kuingiza malipo. 

Kuingiza malipo bila nambari ya risiti kunaweza kusababisha kurekodiwa kwa malipo yasiyolipwa katika mfumo; hatimaye kusababisha taarifa isiyo sahihi ya bakaa ya mkopo na kusababisha athari katika mchakato wa malipo ya mkopo. 

“Napendekeza HESLB ifanyie mapitio na kuimarisha udhibiti wa mfumo katika mchakato wa uhakiki wa malipo ya marejesho ya mkopo ili kuhakikisha kuwa mfumo unathibitisha taarifa zinazoingizwa kwenye mfumo na kuzuia kuingiza malipo bila nambari ya risiti,” amesema CAG. 


Utoaji wa mikopo haya yabainika

Mpango mkakati wa HEASLB ulilenga kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma programu zenye kipaumbele kwa Taifa kwa asilimia 51 ya mikopo yote iliyotolewa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/22. 

Hata hivyo, katika mwaka wa masomo wa 2021/22, asilimia 21 tu ya mikopo, jumla ya Sh33.2 bilioni ilitolewa kwa wanafunzi 14,995 katika maeneo ya kipaumbele ya kitaifa.

Hiyo ni chini ya lengo la asilimia 51 huku Sh156.7 bilioni zilizobaki zililipwa kwa wanafunzi 57,644 katika maeneo mengine, kinyume na miongozo.

Hii inatokana na idadi ndogo ya waombaji walio na sifa za kusomea masomo yanayohusiana na maeneo muhimu ya kipaumbele ya kitaifa, ambayo inaweza kuzuia kufikia malengo ya maendeleo ya kitaifa kutokana na upungufu wa wataalamu na nguvu kazi. 

“Ninapendekeza Serikali iweke misingi sahihi kwa wanafunzi kusoma masomo yanayoendana na vipaumbele vya Taifa,” amesema CAG.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks