Bei ya petroli, dizeli yashuka Dar

Daniel Samson 0147Hrs   Machi 06, 2020 Biashara
  • Wateja wa rejareja wataokoa Sh22 kwa petroli, Sh42 kwa dizeli na Sh2 kwa mafuta ya taa kwa kila lita moja watakayonunua ikilinganishwa na bei ya mwezi uliopita.
  • Mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Dar es Salaam. Wamiliki wa vyombo vya moto watapata ahueni kidogo baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa mwezi Machi 2020.

Ahueni hiyo inakuja baada ya taarifa ya EWURA kueleza kushuka kwa bei za nishati hiyo kwa bei za rejareja na jumla kuanzia Machi 4, 2019) kwa mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam. 

Katika bei hizo mpya, wateja wa rejareja wataokoa Sh22 kwa petroli, Sh42 kwa dizeli na Sh2 kwa mafuta ya taa kwa kila lita moja watakayonunua ikilinganishwa na bei ya mwezi uliopita.

Bei hizo zimepungua kwa viwango tofauti hadi kufikia Sh2,204 kwa lita moja ya petroli, Sh2,153 kwa dizeli na Sh2,116 kwa mafuta ya taa kwa bei za rejareja jijini Dar es Salaam. 

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa viango tofauti. 

“Mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium),” inaeleza taarifa hiyo ya Ewura, 


Soma zaidi: 


Hata hivyo, ahueni hiyo haitawagusa wakazi wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara kwa kuwa bei za mafuta hazijabadilika kwa sababu Bandari ya Tanga haikuingiza shehena mpya licha ya kuwa bei za mafuta zimeongezeka. 

Bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zimeongezeka kwa Sh3 kwa lita sawa na asilimia 10.14. 

Pia bei za petroli na dizeli iliyopitia bandari ya Mtwara inayohudumia mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zimebadilika ikilinganishwa zilizotangazwa Februari 5, 2020, licha ya kuwa hakuna shehena mpya ya mafuta iliyoingia kupitia bandari hiyo. 

Bei za rejareja za petroli imeongezeka kwa Sh46 kwa lita moja, dizeli (Sh35).

Ewura imebainisha kuwa kupanda kwa bei za mafuta katika mikoa hiyo ni “kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji za wafanyabiashara wa mafuta wa jumla na rejareja kutokana na mfumuko wa bei kwa mwaka 2018.”

Aidha, Ewura imesema kwa kuwa hakuna mafuta ya taa yaliyopokelewa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika.

Mafuta ni moja ya bidhaa muhimu katika sekta ya viwanda na uchukuzi na ni miongoni mwa bidhaa ambazo hutumia fedha nyingi katika uingizaji wa bidhaa nchini.

Related Post