Bandari ya Inyala kufungua fursa mpya za kibiashara Nyanda za Juu Tanzania

June 24, 2019 9:31 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • TPA kuanza upembuzi yakinifu mwaka 2019/2020 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo katika eneo la ukubwa ekari 100. 
  • Bandari hiyo ni kwa ajili ya kukabiliana na ushindani wa bandari za nchi jirani na kuhudumia wafanyabiashara wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Dar es Salaam. Katika kuongeza wigo wa biashara na kukabiliana na ushindani wa huduma za bandari na nchi jirani, Serikali inakusudia kujenga bandari kavu katika eneo la Inyala mkoani Mbeya. 

Bandari hiyo itahudumia wafabiashara wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na wateja wa Zambia, Congo DRC na Malawi wanaotumia reli ya Tazara. 

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kukamilisha azma hiyo ikiwemo kutafuta eneo litakalojengwa bandari hiyo. 

“Katika bajeti ya mwaka 2019/2020 TPA (Mamlaka ya Bandari Tanzania) imepanga kufanya upembuzi yakinifu katika eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ili kubaini mahitaji halisi na eneo linalofaa kwa ajili ya kujenga bandari,” amesema Mhandisi Nditiye.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo, uthamini utafanyika na taratibu za kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo zitaanza.

Amesema Ili bandari hiyo itakayojengwa ilete tija, mpango wa Serikali kupitia Tazara ni kufanya upembuzi yakinifu kwa lengo kutandika reli kuelekea katika eneo likalojengwa bandari kavu ya Inyala. 

“Mpango huu unatarijiwa kuanza katika mwaka 2020/2021,” amesema Mhandisi Nditiye leo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza aliyetaka kujua Serikali itaanza lini kujenga bandari hiyo ili kukabiliana na ushindani na nchi jirani. 


Soma zaidi: 


Njeza amesema biashara ya mizigo ya shehena katika maeneo hayo, imepungua kwa asilimia 25 kwa nchi ya Zambia na Congo DRC  imepungua hadi asilimia 21 kutoka asilimia 40. 

Aidha, Nditiye amebainisha kuwa mkakati uliopo ni kuunganisha bandari ya Inyala na Itungi iliyoko Kyela kwa reli ya Tazara ili kuweza kuhudumia nchi za jirani za Congo DRC, Malawi, Zimbabwe na Zambia.

Hata hivyo, mkakati huo utaanza baada ya kukamilika kwa kipande cha reli ya Tazara kitakachounganishwa na bandari kavu ya Inyala.

Enable Notifications OK No thanks