Anna Nkyalu: Ukosefu wa ajira ulivyomfungulia fursa ya kufaidika na kipaji cha uchoraji

March 8, 2021 6:42 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Alianza kutumia kipaji cha kuchora kama ajira mwaka 2019 baada ya kukosa ajira ya ualimu.
  • Kipaji hicho kimemsaidia kutoa elimu kwa jamii na kumuingizia kipato.
  • Pia anakitumia kama nyenzo ya kukabiliana na changamoto za wanawake kwenye jamii. 

Leo Machi 8, 2021 ni Siku ya Wanawake Duniani ambayo inaadhimishwa kutambua mchango wa wanawake katika kuchagiza maendeleo duniani. 

Pia ni siku maalum ya kutathmini mikakati iliyopo ya kumkomboa mwanamke kiuchumi, kifikra na kijamii katika mifumo mbalimbali ukiwemo mfumo dume.

Hata hivyo, wapo baadhi ya wanawake ambao wanazitumia changamoto wanazopitia katika maisha kuzibadilisha kuwa fursa ya wao kuinuka kiuchumi na jamii inayowazunguka. 

Miongoni mwao ni Anna Nkyalu ambaye kitaaluma ni mwalimu aliyehitimu elimu ya juu Tanzania katika masomo ya sayansi. Ukosefu wa ajira ya ualimu imekuwa ni neema kwake kwa sababu kipaji alichozaliwa nacho ndiyo kinambeba kimaisha.

Anna ana kipaji cha kuchora picha za aina mbalimbali zinazoelezea hisia na matukio yaliyopo kwenye jamii. 

Akihojiwa na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam, (UNIC) hivi karibuni, Anna ameeleza kuwa anafanya sanaa ya kuchora michoro mbalimbali lakini anatumia kalamu au peni. 

“Sanaa ya kalamu au peni ni sanaa ambayo watu wengi wanaona ni ngumu kwa sababu unavyotumia kalamu hauwezi kufuta na hata kama ukifuta, inabidi nihakikishe sikosei na hata kama nikikosea basi niyakubali makosa na yawe katika mfumo ambayo yanaweza kuvutia kwa mtazamaji,” anasema binti huyo wakati akihojiwa na UNIC.

Anna ana kipaji cha kuchora picha za aina mbalimbali zinazoelezea hisia na matukio yaliyopo kwenye jamii. Picha| intussein.

Kwa nini kuchora na siyo kufundisha?

Katika mahojiano hayo yaliyorushwa Machi 5 mwaka huu, Anna anasema amekuwa anapenda kuchora tangu akiwa mdogo lakini kuchora hasa kwa ajili ya kipato ilikuja baada ya kukosa ajira alipohitimu chuo kikuu. 

“Nimeanza mwaka 2019 baada ya kumaliza chuo kutokana na changamoto za ajira nikaamua kufanya hii sanaa kama sehemu ya kunipatia kipato. Kama mtu akitokea akitaka nimchoree picha au kama kuna picha nimeichora na mtu akaiona akaipenda akainunua basi ikawa ndiyo sehemu ya kazi yangu,” Anna, akiongea na UNIC. 

Hata hivyo, Anna ana kibarua kigumu cha kujiimarisha kwa sababu changamoto bado ni nyingi ikiwemo watu kuona kazi za kuchora zinawafaa wanaume na siyo wanawake. 

“imeshazoeleka kuwa wasichana hawawezi kufanya vitu vikubwa na vizuri kama wanaume. Akiona unakutana na watu wengi hususan wanaume ni wengi kwenye hii fani, na wasichana ni wachache. 

“Na mtu akiona msichana hakuchukulii uzito au hakuamini. Huku familia nayo inakuwa ina wasiwasi kwamba mtoto wetu vipi huyu anapoteza muda,” anaeleza binti huyo.

Shughuli hiyo siyo haba kwa sababu inampatia kipato za kujikimu kimaisha ambapo bei ya picha hutegemea ukubwa na uzito wa kazi yenyewe lakini kwa watalii huwauzia picha moja kwa kuanzia Dola za Marekani 100 (Sh230,000).


Zinazohusiana:


Alipoulizwa na mwandishi wa kituo cha UNIC kuhusu picha ambayo imemgusa zaidi katika kazi zake zote ambazo amewahi kuzifanya, Anna ametaja picha aliyoipatia jina Komesha Ukatili dhidi ya wanawake.

Picha hiyo inaonyesha sura ya mwanamke akiwa amezibwa mdomo huku vidole vya mkono huo vikiwa vimechorwa maua, fedha na bunduki. 

Binti huyo amekiambia kituo hicho kuwa  “hii picha nimechora kupinga unyanyasaji wa wanawake kwenye jamii yangu, kama unavyoona hapa ni mwanamke amefungwa na pesa, dini, bunduki na maua na zawadi kama upendo ili asiongee kutokana na manyanyaso anayokutana nayo.”

Mchoraji huyo wa picha anaamini kuwa njia rahisi ya kukomesha ukatili wa kijinsia ni watu kuzungumza kwa uwazi mambo yanayowahusu na kutafuta suluhu ya changamoto wanazokutana nazo badala ya kukaa kimya. 

Tunawatakiwa kila heri wanawake wote duniani katika siku hii muhimu na wafahamu kuwa dunia iko pamoja nao na inatambua mchango wanauotoa katika kusongesha gurudumu la maendeleo.

Enable Notifications OK No thanks