Ahueni: bei za petroli, dizeli zikishuka Tanzania

Rodgers George 1055Hrs   Mei 05, 2020 Biashara
  • Wateja wa rejareja wa Dar es Salaam  wataokoa Sh219 kwa petroli na Sh143 kwa dizeli.
  • Ahueni hiyo pia itaendelea kuwanufaisha wakazi wa mikoa ya Tanga na mikoa mingine ya Kaskazini ambako nishati hiyo imeshuka.
  • Kushuka kwa bei za mafuta kunatokana na mabadiliko katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Dar es Salaam. Wamiliki wa vyombo vya moto watapata ahueni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kwa mwezi Mei 2020.

Ahueni hiyo inakuja baada ya EWURA kueleza kushuka kwa bei za nishati hiyo kwa bei za rejareja na jumla kuanzia kesho (Mei 6, 2020) kwa mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam. 

Katika bei hizo mpya, wateja wa rejareja wataokoa Sh219 kwa petroli, Sh143 kwa dizeli na Sh355 kwa mafuta ya taa kwa kila lita moja watakayonunua ikilinganishwa na bei zilizotumika mwezi uliotangulia wa Aprili.

Kwa upande wa bei za jumla, bei zimepungua kwa Sh218.59 kwa lita moja ya petroli, Sh142.25 kwa mafuta ya dizeli huku mafuta ya taa yakipungua kwa 354.09.

“Mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium) ,” inaeleza taarifa hiyo ya Ewura.

Nafuu hiyo itawagusa pia wakazi wa mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania ya  Tanga, Arusha, Killimanjaro na Manyara baada ya bei za nishati hiyo muhimu kwa usafiri kushuka ikilinganishwa na toleo lililopita.

Wakazi wa mikoa hiyo watapata ahueni kwa Sh463 kwa lita moja ya petroli na Sh377 kwa lita moja ya mafuta ya dizeli. 

Kwa wauzaji wa bei za jumla watauza mafuta hayo kwa pungufu ya Sh 461.82 kwa lita moja ya petroli na Sh375.82 kwa lita moja ya dizeli.

Hata hivyo, kwa mikoa hiyo, bei ya mafuta ya taa itaendelea kuwa ile ile kama ilivyotumika mwezi Aprili.


Zinazohusiana


Kwa upande wa mikoa ya Kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma) bei ya mafuta ya dizeli hazitabadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Aprili kutokana na kuwa hakuna shehena ya dizeli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara. 

Bei za rejareja za petroli zimeshuka kwa Sh129 kwa lita na Sh128 kwa bei ya jumla na Sh128 kwa bei ya jumla. 

“Kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika,” imesomeka taarifa ya Ewura.

Mafuta ni moja ya bidhaa muhimu katika sekta ya viwanda na uchukuzi na ni miongoni mwa bidhaa ambazo hutumia fedha nyingi katika uingizaji wa bidhaa nchini.

Related Post