Ahueni, maumivu: Bei ya mchele yapanda Tanzania

January 13, 2022 2:19 pm · Maria
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mchele kwa mwaka ulioishia Novemba 2021 ilikuwa Sh154,395 ikiwa imepanda kutoka Sh144,332 iliyorekodiwa Novemba 2020.
  • Gharama za usafiri, kuadimika kwa mchele vyachangia bei kupanda.
  • Wanunuzi kuendelea kuumia, wakulima wakichekelea.

Dar es Salaam. Wakati wakulima mahindi wakilia kushuka kwa bei ya zao hilo, wenzao wanaojishughulisha na mchele ni kicheko kwa sababu bei ya zao hilo imepanda kwa asilimia saba ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi December 2021 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2021 ilikuwa Sh49,683 ikiwa imeshuka kutoka Sh58,012 iliyorekodiwa Novemba 2020.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa wastani wa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mchele kwa mwaka ulioishia Novemba 2021 ilikuwa Sh154,395 ikiwa imepanda kutoka Sh144,332 iliyorekodiwa Novemba 2020.

Bei hiyo ya Novemba mwaka jana ni kubwa kwa asilimia saba zaidi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia mwezi Novemba. 

Hii ina maana kuwa mkulima aliyeuza mchele Novemba mwaka jana alipatata malipo zaidi kwa Sh10,063 kwa gunia la kilo 100 ikilinganishwa na alivyouza kipindi kama hicho mwaka juzi. 

Kupanda kwa bei hiyo ya mchele kunawanufaisha zaidi wakulima na kuwaumiza wanunuzi hasa walaji kwa kuwa wanalazimika kutoboa zaidi mifuko yao kupata chakula hicho muhimu.

Lakini wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo, kwao ni furaha kubwa kwa sababu inawaongezea faida ambayo wanapata wanapouza kwa bei hiyo ya juu ukilinganisha na ile waliyouza Novemba 2020.

Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo za BoT unaonyesha kuwa bei ya zao hilo imeendelea kupanda kwa miezi ya minne mfululizo tangu Agosti mwaka jana.

Mwezi Agosti mwaka jana bei ya jumla ya mchele ilikuwa Sh140,136, ikapanda mwezi uliofuata hadi Sh141,520.2 na mwezi Oktoba ikafikaSh151,887.8 kabla haijafika  Sh154,395 mwezi Novemba.


Zinahusiana: 


Mchele wa rejareja nao wapanda

Kupanda kwa bei ya mchele pia kumeendelea kujidhihirisha katika maeneo mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam.

Mfanyabiashara wa mchele katika soko la Mwananyamala jijini Dar es salaam, Samson Lazaro amesema kupanda kwa bei ya zao hilo  kunawaumiza pia nao wao kutokana na gharama kubwa za usafiri wanazotumia kutafuta na kufikisha mzigo sokoni. 

“Shambani hakuna mchele lakini pia wakulima walishahifadhi mchele mapema kwa kujua kwamba miezi michache ijayo kutakua na uhitaji zaidi wa zao hilo, ninazunguka hata zaidi ya wiki mbili kutafuta mchele na ndomana stoo yangu imekauka kabisa,” amesema Lazaro wakati kiongea na Nukta Habari.

Gharama hizo za usafiri pia zimechangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo hutumika kuendesha vyombo vya usafiri.

Kwa mujibu wa bei zinazotumika leo Januari 13 katika soko la Mwananyamala, mchele umepanda bei kiasi kwamba ule aliokuwa akiuza Sh1400 sasa hivi anauza Sh1700 na ule wenye ubora wa juu zaidi ambao awali aliuzwa kwa Sh1700 hadi Sh1800, sasa hivi anauzwa kwa Sh2200 mpaka 2400.

Mfanyabiashara huyo anasema kwa sasa matumaini ya kushuka kwa bei za mchele ni madogo labla mpaka msimu wa mavuno.

“Kwa kweli matumaini ya kupungua bei ya mchele hayaonekani kwasababu mchele ndio unazidi kuadimika tunalazimika kutumia wiki nzima kutafuta mchele ukipata ukauleta sokoni huwezi kuuza bei ile ile,” amesema Lazaro.

Kutokana na mabadiliko hayo ya bei, mfanyabiashara huyo anadai kuwa anakumbana sana na changamoto za wateja kutokana na kwamba duka lake lipo mbele hivyo mteja anaweza kufika akazani ni hapo tu bei ni kubwa na kufanya wateja kuendelea mbele ili kuangalia bei ya mchele katika maduka mengine.

“Wateja wangu wengi sana wanalalamika bei ya mchele ipo juu,” amesema Lazaro.

Pia bei ya mazao mengine ya chakula ikiwemo uwele na mtama zilipanda ndani ya mwaka mmoja uliopita unaoishia Novemba isipokuwa mahindi, viazi mviringo na maharage.

Uwele ulipanda hadi Sh105,371 mwaka ulioshia mwezi Novemba 2021 kutoka Sh88,439 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka juzi.

Enable Notifications OK No thanks