Rais Samia ateua, atengua na kuhamisha wakuu wa wilaya, makatibu tawala wilaya

January 24, 2025 7:02 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ateua wakuu wa wilaya wapya watano, wengine saba wabadilishiwa vituo vya kazi mmoja atenguliwa.

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi, uhamisho na mabadiliko ya viongozi mbalimbali ikiwemo wakuu wa wilaya 12 na makatibu tarafa watano. 

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka, iliyotolewa leo Januari 24, 2025 inabainisha kuwa miongoni mwa walioteuliwa ni Godfrey Mnzava Afisa Tarafa ya Ilemela aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi. 

Uteuzi wa Mnzava utajaza nafasi iliyoachwa wazi na James Wilbert Kaji  aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa  (NIDA) Desemba 18, 2024.

Aidha, Rais Samia amefanya uteuzi wa viongozi wengine wawili watakaochukua nafasi za wakuu wa wilaya za Mbulu na Ulanga ambao wamestaafu.

“Michael John Semindu, Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa ameteuliwa kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Mbulu kuchukua nafasi ya Bi. Veronica Arbogast Kessy ambaye  amestaafu…

…Khamana Juma Simba, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha ameteuliwa kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Ulanga kuchukua nafasi ya Dkt. Julius Keneth Ningu ambaye  amestaafu,” imesema taarifa ya Kusiluka.

Wengine walioteuliwa kushika nafasi ya ukuu wa wilaya ni pamoja na Hamad Mbega, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama aliyeteuliwa kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Mbozi na Peter Masindi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu.

Pamoja na hao Rais Samia amewabadilishia vituo vya kazi wakuu wa wilaya wengine saba akiwemo Joseph Mkude kutoka Wilaya ya Kishapu kwenda Wilaya ya Arusha akuchukua nafasi ya Felician Mtahengera ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Joachim Thobias Nyingo amehamishwa kutoka Wilaya ya Kilolo kwenda kuwa  Wilaya wya Bahi wakati Rebecca Msemwa amehamishwa kutoka Wilaya ya Bahi kwenda Wilaya ya Kilolo.

Wengine waliohamishiwa vituo vya kazi ni Hassan Bomboko kutoka Wilaya ya Ubungo kwenda Wilaya ya Hai, Lazaro Twange (kutoka Wilaya ya Hai kwenda Wilaya ya Ubungo), Kisa Kasongwa (kutoka Wilaya ya Njombe kwenda Wilaya ya Makete) na Juma Sweda kutoka Wilaya ya Makete kwenda Wilaya ya Njombe. 

Rais ateua makatibu tawala wa wilaya watano

Katika hatua nyingine Rais Samia ameteua makatibu tawala wa wilaya wanne na kumbadilishia kituo Jacob Rombo kutoka Wilaya ya Mbogwe kwenda Wilaya ya Arusha

Jacob anakwenda kuchukua nafasi ya Khamana Simba ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga. 

Wengine walioteuliwa kuwa makatibu tawala wa wilaya ni pamoja na Benard Urasa, Afisa Tawala Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa (Tamisemi) aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa akichukua  nafasi ya Michael Semindu.

Francis Faty, Mhadhiri Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe kuchukua nafasi ya Jacob   aliyehamishiwa kituo cha kazi

Happyness Sulle, Mkuu wa Kitengo cha Maktaba na Nyaraka wa Chama cha  Mapinduzi (CCM) ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama huku Glory Absalum, Afisa Tarafa ya Bashnet, Babati akiteuliwa kuwa Katibu Tawala  wa Wilaya ya Kahama kuchukua nafasi Hamad Mbega.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks