Mazoezi yanayoweza kuongezea ufanisi kazini

August 21, 2019 2:07 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mazoezi yote yanaweza kufanyika ndani ya dakika 30 na zaidi.
  • Faida ya mazoezi haya ni pamoja na kuchangamsha mwili na kuondoa mafuta yasiyohitajika mwilini.
  • Unaweza kufanya ukiwa nyumbani bila kwenda “Gym”.

Dar es Salaam. Baada ya kukuletea shughuli ndogo ndogo ambazo unaweza kufanya ukiwa ofisini kwa ajili ya kuepukana na madhara yanayotokana na kukaa kwa muda mrefu ikiwemo kisukari, kiharusi, presha na hata kitambi, sasa tunakuletea mazoezi rahisi ambayo unaweza kuyafanya uwapo nyumbani kwa muda ya dakika 30 hadi 45.

Kwa mujibu wa Dk Joshua Sultan ambaye ni Mfiziotherapia, kufanya mazoezi haya kila siku kama ukiweza au mara nne kwa wiki, itakupunguzia maumivu ya mgongo ambayo yanatokana na kukaa mkao usio sahihi kwa muda mrefu hasa ukiwa ofisini.

Dead bug

Hili zoezi linatuliza misuli ikiwemo ya mikono na tumbo na hata mgongo. Kulifanya zoezi hili unahitaji kulala chini kwa mtindo wa chali huku ukinyoosha miguu na mikono kuelekea juu. Hakikisha unakua umetengeneza mfano wa meza iliyogeuzwa na ni vyema miguu na mikono vikanyooka kwa digrii 90.

Anza kushusha chini mguu wa kulia sambamba na mkono wa kushoto lakini usiguse chini kisha rudia hali ya mwanzo wa zoezi na kisha fanya hivyo hivyo na mguu wa kushoto na wa kulia. Fanya hivyo mara 20 kwa kila upande.

Hili ni miongoni mwa zoezi rahisi unaloweza kufanya ukiwa nyumbani. GIF|Self

Plank

Hili zoezi linagusa mwili mzima hasa misuli ya msingi “core muscles”. Kwa mujibu wa Dendee Kichamo ambaye ni mwalimu wa mazoezi kutoka “Afya Gym” iliyopo Boko jijini Dar es Salaam, Plank inafanywa na mtu yeyote.

Kufanya zoezi hili mtu anahitaji kulala chini na kufanya kama anapiga “push up” ila tu wa upande wa mikono, mtu anahitajika kulaza mkono kutokea kwenye kiwiko. 

Hakikisha kuwa mwili umenyooka wakati wa kufanya zoezi hili na ganda kwa muda wa sekunde 30 tu. 

Zoezi hili pia litakusaidia kupunguza tumbo. Picha|Self

Deadlifts 

Kufanya zoezi hili, unahitaji kuwa na kitu kizito, Kichamo anasema ni busara kupima uzito wako na kisha kumuuliza daktari au mwalimu wa mazoezi juu ya uzito unaostahili kufanyia mazoezi.

Kufanya zoezi hili unahitaji kuachanisha miguu yako kidogo na kisha beba kifaa chako chenye uzito ambacho kitaalamu kinaitwa “dumbell” huku ukiwa umenyoosha mikono yako kuelekea chini, fanya kama unachuchumaa pasi kufika chini.

Amesema zoezi hili ni zuri kwa mgongo, mapaja na miguu na hata mabega na mikono.


Zinazohusiana:


Kuruka kamba

Kuruka kamba kunamsaidia mtu kuondoa mafuta mwilini na pia inamfanya awe fiti. Pia inawezesha kuupa mwili kazi baada ya kukaa kwa siku nzima.

Kichamo anasema kuwa zoezi hilo linatakiwa kufanywa hadi pale mtu atakapotoa jasho.

“Ili kujua kuwa umeanza kufanya mazoezi, ni muhimu uone jasho linachuruzika,” anasema Kichamo. 

 Kuruka kamba nayo ni njia nyingine ya kuboresha afya yako. GIF|Self.

Squats

Zoezi hili ni rahisi sana japo kwa mujibu wa Kichamo, linaweza kukusababishia maumivu kwenye mapaja na mara baada ya mwili kuzoea, mtu anarudi katika hali ya kawaida.

Kufanya zoezi hili unahitaji kuachanisha miguu kidogo na kisha kuweka mikono kwa namna utakayokuwa huru. Unaweza kushika kiuno au ukainyoosha mikono kuelekea kifuani na kisha shuka taratibu kama unachuchumaa unaweza rudia zoezi hili mara 15 au zaidi.

Pia unaweza badilisha zoezi na kulifanya kwa staili ya kupishanisha miguu Ili zoezi lifanye kazi vizuri, mara kadhaa ishia katikati wakati unachuchumaa na kisha ganda kwa sekunde 30 ama hata dakika moja.

Kufanya zoezi hili unahitaji kuachanisha miguu kidogo na kisha kuweka mikono kwa namna utakayokuwa huru. GIF|Self.

“Mazoezi mengi kama kata tumbo, squat na mengine yanaweza kumpa tabu mtu mwanzoni lakini akishazoea anaendela vizuri,” amesema Kichamo. 

Kwa mazoezi haya unayoweza kufanya ukiwa nyumbani, yatakusaidia kukabiliana na uchovu na maumivu ya mwili ukiwa kazini. 

Enable Notifications OK No thanks