Rais Samia, viongozi wachambua maisha ya mzee Mkapa
Rais Samia Suluhu Hassan amefungua Kongamano la Kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa (1St Mkapa’s Legacy Symposium) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam leo Julai 14, 2021. Picha| Ikulu Tanzania.
- Wasema kitabu cha historia ya Tanzania hakiwezi kukamilika bila ya Mzee Mkapa
- Wasema alikuwa kiongozi shupavu na mzalendo.
- Wamesema wataendelea kumkumbuka daima.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kitabu cha historia ya Tanzania hakiwezi kukamilika bila kuwepo sura nzima itakayomwelezea Hayati Rais Benjamin Mkapa kutokana na mchango wa kiuongozi aliouacha nchini ikiwemo mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya katika uongozi wake.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa hauli hiyo alipokuwa anafungua Kongamano la Kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa (1St Mkapa’s Legacy Symposium) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam leo Julai 14, 2021.
“Wakati wa uongozi wake Mzee Mkapa alisimamia mageuzi ya uchumi kwa kutoa fursa kwa sekta binafsi na kukaribisha uwekezaji kutoka nje na hatua hizi zilisaidia kuongeza mapato ya Serikali kutoka Sh331.2 bilioni mwaka 1995 hadi kufikia Sh2 trilioni mwaka 2005,” amesema Rais Samia.
Sifa nyingine ya Mzee Mkapa ni uwezo wake mkubwa wa kutokuogopa mijadala ya kimataifa na kutekeleza kile alichokiamini hata kama
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000 kulikuwa na vuguvugu kubwa la kupinga masuala ya utandawazi, Mzee Mkapa hakufuata mkumbo badala yake alijitokeza hadharani kuutetea na kueleza kwanini tunapaswa kuupokea.
“Siku zote ni vigumu kuzungumza mwisho hasa baada ya wazee wote hawa kuzungumza, nimewasikiliza kwa makini wale wote waliowahi kufanya kazi na kumfahamu kwa ukaribu zaidi Hayati Mkapa, wamemwelezea kama kiongozi aliyekuwa na maono makubwa,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan akifungua Kongamano la Kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa (1St Mkapa’s Legacy Symposium) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam leo Julai 14, 2021. Picha| Ikulu Tanzania.
Awali Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Katika kipindi chote cha maisha ya Hayati Benjamin Mkapa kama mtumishi wa umma aliweka huduma kwa wananchi kama kipaumbele cha kwanza kwenye ajenda yake, na kwamba alikuwa ni mtu mwenye maono, mzalendo, mchapakazi na aliyejua kujieleza vizuri.
“Ninampongeza Kaka yangu, rafiki na mwalimu wangu Hayati Benjamin Mkapa kwa kuanzisha taasisi ambayo imekuwa ikitukumbusha kuhusu mtu aliyekuwa nyuma ya maono hayo kupitia kazi zinazotekelezwa, tutamkumbuka daima na tutaendelea kuishi kupitia urithi wake,” amesema Rais Mstaafu Kikwete.
Amesema wakati wa utawala wake alikumbana na changamoto ya upatikanaji wa wafanyakazi wa sekta ya afya kwenye maeneo yenye mazingira magumu lakini Taasisi ya Benjamin Mkapa ilikuja kushirikiana na Serikali na kuleta ufumbuzi.
Anasema waliweza kupata zaidi ya wafanyakazi 1,900 waliosaidia kuleta mafanikio kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair amesema alimfahamu Hayati Benjamin Mkapa kupitia kazi zake nzuri alizokuwa akizifanya na kwamba alikuwa na mapenzi makubwa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla na alijidhatiti katika kuiletea maendeleo nchi yake.
Amesema anajua huko aliko anajivunia sana kuona namna Taasisi ya Benjamin Mkapa inavyofanya kazi kwa niaba yake.
“Ukaribu na urafiki uliokuwepo kati yangu na Mkapa ni moja ya mambo ambayo ninayathamini sana katika maisha yangu, ni imani yangu watu wote waliomfahamu walifurahia kufanya naye kazi kwani alikuwa mtu mwema na mwenye maono mapana,” amesema Blair.
Latest
