Serikali yazindua sera mpya ya elimu na mafunzo kukabiliana na ukosefu wa ajira, kukuza uchumi

February 1, 2025 5:22 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanafunzi kusoma elimu ya msingi ya lazima kwa miaka 10 ikiwawezesha kujiajiri, kuajiriwa.
  • Rais Samia asisitiza utekelezaji wa sera pamoja na mitaala mipya.

Arusha. Serikali ya Tanzania imezindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 itakayochochea mabadiliko katika mifumo ya elimu nchini yatakayoongeza uwezo wa vijana kujiajiri na kukuza uchumi.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa sera hiyo leo Februari 1, 2025 amesema kuwa lengo la kufanya maboresho ya sera hiyo ni kumuandaa kijana wa kitanzania mwenye uwezo na ujuzi unaohitajika.

“Dhamira yetu ni kumuandaa kijana anayejiamini na mwenye nyenzo stahiki za kukabiliana na ushindani wa kikanda na kimataifa ili kwa kutumia utajiri wa rasilimali zetu aweze kunufaika kiuchumi,” amesema Rais Samia.

Maboresho ya sera hiyo yamefanyika ili kukabiliana na changamoto zilizokuwa zinaukumba mfumo wa elimu nchini ikiwemo kuzalisha wataalamu wasiokuwa na ujuzi pamoja na ukosefu wa ajira.

Kwa kutambua changamoto hizo Serikali iliunda kamati maalum ya kupitia sera hizo pamoja na kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali waliowezesha kukamilika kwa toleo la kwanza la maboresho ya sera hiyo Ocktoba 2023.

Kutokana na maboresho hayo mapya, hivi sasa elimu ya msingi (ya lazima) itatolewa kwa miaka 10 tofauti na miaka saba ya awali ambapo mwanafunzi atatakiwa kuanza shule akiwa na miaka sita.

Baada ya elimu ya msingi mwanafunzi ataenda elimu ya sekondari ya upili (advanced education) ambapo atatakiwa kuchagua kati ya mkondo rasmi au mkondo wa amali kisha baada ya hapo anaweza kuendelea na elimu ya chuo kikuu.

Kwa upande wa elimu ya amali mwanafunzi atachagua kozi moja kati ya kozi 15 zitakazotolewa ambazo ni pamoja na uhandisi umeme na mitambo, ushoni, kilimo, ufugaji na usindikaji chakula na akimaliza atapata cheti kitakachomuwezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Rais Samia amesema kuwa miongoni mwa sababu za kuongeza umri wa elimu ya lazima ni kumuandaa kijana kuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.

“Kupitia sera hii mtoto akianza shule akiwa na miaka sita wakati anahitimu elimu ya msingi ya lazima kwa miaka 10 atakuwa na umri wa miaka 16 hapo atakuwa amemaliza kidato cha nne, umri ambao atakuwa na uwezo wa kuajiri au hata kuajiriwa hivyo kuingia kwenye uzalishaji  moja kwa moja…

…Kwa sababu atakuwa katika mapito yake ya elimu amepata elimu ya amali atakuwa na uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuboresha sera hiyo ili kuendana na mahitaji ya miaka ijayo.

“Sasa tunajiandaa kwa utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2050 yote haya yanalazimu kuwepo kwa sera mpya ya elimu itakayoashiria mwanzo wa ng’we mpya katika safari ya kuimarisha, kuendeleza elimu yetu kufikia viwango vya juu vinavyokidhi ubora unaohitajika,” amesema Kikwete.

Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Elimu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wa mitaala hiyo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

“Uwepo wa mitaala na sera peke yake haiwezi kuleta matokeo tunayotaka kitakacholeta utofauti ni utekelezaji wa sera yenyewe …kila mmoja wetu atimize wajibu wake, watoto wahudhirie masomo watoto wahakikishe wanafuatilia mwenendo wa watoto wao na sisi Serikali tuendelee kudhibiti ubora,” amesema Rais Samia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks