Marekani yaomboleza vifo vya wanajeshi wa JWTZ Kongo
- Yatoa pole kwa JWTZ, wanafamilia na Watanzania.
- Yasema inasikitishwa na ongezeko la mzozo mashariki mwa Kongo.
Dar es salaam. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa pole kwa Serikali kufuatia vifo vya wanajeshi wake wawili wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliofariki katika mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Licha ya kutoa pole kwa JWTZ, familia za marehemu na Watanzania kwa ujumla taarifa iliyotolewa na ubalozi huo na kuchapishwa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii imeeleza kuwa inasikitishwa na kuongezeka kwa mzozo unaoendelea Mashariki mwa Kongo hususan Goma.
“Marekani inasikitishwa sana na kuongezeka kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo(DRC), hasa kwa Goma kuwa mikononi mwa kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda, na inasisitiza kusitishwa mara moja kwa mapigano katika eneo hilo, na kwa pande zote kuheshimu mipaka ya nchi,” inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ Kanali Gaudentius Ilonda vifo vya wanajeshi hao vimetokea kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliyofanywa na waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari 2025 ambapo askari wengine wanne wamejeruhiwa.
https://x.com/JKTonlinetz/status/1886155184432160821
JWTZ imeeleza kuwa jitihada za kusafirisha miili pamoja na majeruhi zinaendelea kutekelezeka kupitia sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Hata hivyo, taarifa hiyo imeeleza kuwa vikundi vingine vilivyopo nchini DRC vipo salama na vina endelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC.
“Vikundi vilivyopo DRC vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kupitia majukumu yake kwa maelekezo ya SADC” imeeleza taarifa hiyo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa SADC zilizopeleka askari wake kusaidia kudhibiti mapigano kati ya Jeshi la Kongo na waasi wa M23 ambao wiki iliyopita waliripotiwa kuutwaa mji wa Goma.