Fahamu faida za ulaji wa brokoli

February 18, 2025 6:58 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuzuia ugonjwa wa moyo na kuimarisha afya ya mifupa kulingana na uwepo wa nyuzi nyuzi na vitamini.
  • Kusaidia mmeng’enyo wa chakula na matatizo ya kiungulia.

Dar es Salaam. Kuna aina za nyingi za mbogamboga na kila moja ina faida zake katika mwili wa binadamu ikiwemo kuimarisha kinga mwilini.

Pamoja na wingi wa mboga hizo, kila moja ina faida zake mahususi ambazo unaweza usizipate katika aina nyingine za mboga au ukazipata kwa uchache.

Katikati ya aina hizo za mboga ipo brokoli, mboga maarufu inayosifika kwa faida nyingi za kiafya ikiwemo wingi wa kirutubisho adimu cha vitamini K ambacho hakipatikani kwenye mboga nyingi.

“Ni miongoni mwa mmea wenye vitamini C nyingi, vitamini K ambayo ni ‘very rare’ (adimu sana) kuipata. Vitamini K inapatikana kwenye vyakula vichache, ina madini ya chuma, vitamini D, A. 

…Lakini pia ina madini mengi ina kalsium, magnesium, potassium,” amesema  Irine Kweka,  Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Kondoa jijini Dodoma.

Hata hivyo, Kweka ameongeza kuwa sifa kubwa ya brokoili uwepo wa  antioxidanti nzuri kulingana na uwepo wa vitamini.

Kwanini ule brokoli?

Brokoli husaidia kupunguza viwango vya lehemu (cholesterol) mbaya (LDL) na kuongeza lehemu nzuri (HDL).Picha/Nutrition and Health Innovation Research Institute.

Ikiwa bado unajiuliza sababu za kuongeza brokoli katika mlo wako wa kila siku Kweka aliyekuwa akizungumza na Nukta Habari amebainisha kuwa moja aya faida ya kutumia mboga hiyo katika mlo ni kusaidia mmeng’enyo wa chakula kulingana na wingi wa nyuzinyuzi.

Nyuzi nyuzi hizo pia husaidia tatizo la choo kigumu, kudhibiti kiwango cha asidi kwenye tumbo, kukabiliana na kiungulia au vidonda vya tumbo,pamoja na kuongeza idadi ya bakteria wazuri tumboni, ambao ni muhimu kwa usagaji bora wa chakula. 

Bakteria hawa husaidia kuvunjavunja chakula kwa ufanisi na pia huchangia katika afya bora ya kinga ya mwili. 

Kuzuia magonjwa ya moyo

Ulaji wa Brokoli husaidia kupunguza viwango vya lehemu (cholesterol) mbaya (LDL) na kuongeza lehemu nzuri (HDL), hali inayosaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya,  Medical News Today brokoli ina nyuzi nyuzi, antioksidanti, na kemikali za kibaolojia zinazopunguza kiwango cha ehemu na kudumisha utendaji mzuri wa moyo. 

Juisi ya brokoli inaweza kusaidia kudhibiti ugonjwa wa kisukari na hata kuuzuia kabisa. Picha/ Daily Express.

Uwepo wa nyuzi nyuzi hizo kwa wingi, husaidia kuzuia kuziba kwa mishipa ya damu kwa kupunguza kiasi cha mafuta mabaya mwilini hali inayoweza kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu, kiharusi, na mshtuko wa moyo.

Kuimarisha afya ya mifupa

Tovuti ya Naturmed Scientific inaeleza kuwa mifupa yenye nguvu inahitaji virutubisho muhimu kama vile kalsiamu, fosforasi, na vitamini K, vyote ambavyo hupatikana kwa wingi katika brokoli. 

Vitamini K inasaidia katika mgandisho wa damu na pia huchangia uimarishaji wa madini kwenye mifupa, jambo ambalo linapunguza uwezekano wa mifupa kuwa dhaifu au kuvunjika kwa urahisi.

Mifupa yenye nguvu inahitaji virutubisho muhimu kama vile kalsiamu, fosforasi, na vitamini K ambavyo pia hupatikana kwenye brokoli. Picha/ La Muscle.

Pia, brokoli ina kiasi kikubwa cha madini ya magnesiamu na zinki, hali inayowafanya walaji wa brokoli kupunguza msongamano wa mifupa (osteoporosis), unaochangia mifupa kuwa dhaifu na rahisi kuvunjika.

Kinga dhidi ya saratani

Taasisi ya kansa ya nchini Marekani (National Cancer Institute) inabainisha kuwa brokoli ina kemikali zinazozuia ukuaji wa seli zenye uwezo wa kusababisha saratani. 

Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa ulaji wa mara kwa mara wa mboga za jamii ya ‘cruciferous’, ikiwemo brokoli, unaweza kupunguza hatari ya saratani ya matiti, saratani ya tezi dume, na saratani ya utumbo mpana.

Mboga hizi ni za kipekee kwa namna nyingi kimuundo wa kemikali, ikiwa ni pamoja na kiwango chao cha juu cha misombo yenye salfa inayoitwa glukosinolati, ambayo huwapa harufu yao ya kipekee. Picha/ Everyday Health.

Mbali na kinga dhidi ya saratani, brokoli pia inasaidia wagonjw wa saratani  kupunguza madhara yanayotokana na matibabu kama mionzi na dawa za kemikali.

 Kuimarisha afya ya ngozi

Ngozi yenye afya inahitaji lishe bora, na brokoli ni moja ya vyakula vinavyotoa virutubisho muhimu kwa ngozi. 

Vitamini C inayopatikana kwa wingi kwenye brokoli inasaidia mwili kutengeneza collagen, ambayo ni protini muhimu kwa uimara na mng’ao wa ngozi.

Brokoli ina nguvu za ustawi wa mwili kwa kiwango cha nyuzi joto 360º, ikisaidia afya ya moyo, ngozi, na nywele. Picha/ Wild Element.

Brokoli pia ina vioksidishaji vinavyosaidia kupunguza athari za miale ya jua ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa ngozi  huku vitamini A na E, vilivyopo katika mboga hiyo ambavyo vikiifanya ngozi kuwa naunyevu wa kutosha. 

 Kudhibiti sukari ya damu

Kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari, brokoli ni moja ya vyakula vinavyopaswa kujumuishwa katika lishe. Ina misombo inayosaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu kwa kupunguza upinzani wa insulini.

Uwepo wa sulforaphane inayopatikana kwenye brokoli inaweza kusaidia kupunguza viwango vya sukari kwa wagonjwa wa kisukari aina ya pili. 

Nyuzinyuzi zilizopo kwenye brokoli husaidia kuzuia kuongezeka kwa ghafla kwa kiwango cha sukari baada ya kula. Picha/Times of India.

Sulforaphane husaidia kongosho kutoa insulini kwa ufanisi zaidi na hivyo kudhibiti sukari mwilini.

Mbali na hayo, nyuzinyuzi zilizopo kwenye brokoli husaidia kupunguza kasi ya mmeng’enyo wa wanga, na hivyo kuzuia kuongezeka kwa ghafla kwa kiwango cha sukari baada ya kula. 

Hii ni muhimu kwa watu wanaotaka kudhibiti uzito na kuepuka hatari ya kupata kisukari.

Kusaidia kuzuia mchakato wa kuzeeka

Mchakato wa kuzeeka kwa kiasi kikubwa unahusishwa na mkazo wa oksidativi na kupungua kwa kazi ya kimetaboliki wakati wa maisha ya binadamu.

Ingawa kuzeeka ni mchakato wa asili usioepukika, ubora wa lishe unadhaniwa kuwa na mchango mkubwa katika kuamua jinsi jeni zinavyotumika na maendeleo ya magonjwa yanayohusiana na umri 

Matumizi ya mboga hii kwa wingi husaidia kupunguza kasi ya uzee. Picha/Nature4Nature.

Ili kuhifadhi virutubisho vyake, ni vyema kupika brokoli kwa muda mfupi kwa kutumia njia kama kuipika kwa mvuke au kuitumia katika saladi. Kwa kuongeza brokoli katika lishe yako ya kila siku, unaweza kufurahia afya bora na kuzuia magonjwa mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks