Rais Samia afanya uteuzi wa viongozi sita
- Prof Hozen Kahesi Mayaya na Prof Aurelia Kamuzora ni viongozi waliteuliwa kushikilia nafasi zao kwa mara ya pili.
- Dk Habib Galuss Kambanga amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi watano na kumpangia kituo kipya cha kazi Balozi Dk Habib Galuss Kambanga.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka, iliyotolewa leo Februari 13, 2025 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar imewataja viongozi walioteuliwa kuwa ni pamoja na Dk Amina Suleiman Msengwa ambaye aliyeteuliwa kuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Kabla ya uteuzi huu, Dk Msengwa alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua nafasi ya Dk Albina Chuwa ambaye amemaliza muda wake.
Viongozi wengie walioteuliwa ni Jaji Dk Ntemi Kilekamajenga aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Masoko na Mitaji akichukua nafasi ya Jaji Dk Deo John Nangela ambaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Kwa upande wa Prof Aurelia Kamuzora ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa ambapo anashikilia nafasi hii kwa kipindi cha pili sasa.
Abdulmajid Nsekela ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania akichukua nafasi ya Mustafa Hamis Umande ambaye amemaliza muda wake.
Naye, Prof Hozen Kahesi Mayaya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) ambapo amekuwa akikaimu nafasi hii kwa mara ya pili.
Balozi Dk Habib Galuss Kambanga amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.
Dk Kambanga aliteuliwa Juni 15, 2024 wakati huo alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.
Latest



