Rais Samia kuhudhuria mkutano wa G20 Brazil

November 15, 2024 8:40 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kufuatia mualiko wa Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva.
  • Rais Samia kushiriki mijadala ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kufanya mazungumzo na wakuu wa taasisi za kifedha.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Brazil kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 utakaofanyika Novemba 18 – 19, 2024 jijini Rio de Janeiro.

G20 ni nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani na zinazojumuisha takriban theluthi tatu ya idadi ya watu duniani ikiwemo Marekani, China, Urusi, Ujerumani, Brazil pamoja na Ufaransa ambapo viongozi wa nchi hizo hukutana mara mbili kila mwaka, kwa lengo la kujadili masula ya uchumi wa dunia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Novemba 15, 2024 Rais Samia amealikwa na Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva ambaye ndiye Mwenyekiti wa G20 kushiriki mkutano wa jukwaa hilo lenye lengo la kukuza ushirikiano wa kimataifa kwenye masuala ya kiuchumi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuhudhuria katika mkutano wa G.20, ambapo awali marais waliopita wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Benjamin Mkapa kwa nyakati tofauti waliwahi kuhudhuria mkutano kama huo ila uliozikutanisha nchi nane pekee ukiitwa G8.

Taarifa ya Ikulu imebainisha kuwa pamoja na mambo mengine katika mkutano huo Rais Samia anatarajia kushiriki mijadala inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa na umasikini, kuchochea maendeleo endelevu na matumizi ya nishati mbadala.

“Rais Dkt. Samia anatarajia kutumia jukwaa hilo linalokutanisha nchi zenye chumi kubwa zaidi duniani kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kujenga maendeleo endelevu na kutafuta fursa za ushirikiano zitakazowaletea ustawi Watanzania kupitia sekta za uzalishaji,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, akiwa nchini Brazil, Rais Samia atafanya mikutano ya pembezoni na taasisi kubwa za kifedha duniani pamoja na kukutana kwa mazungumzo na wakuu wa nchi na Serikali pamoja na baadhi ya nchi wanachama wa G.20 akiwemo mwenyeji wake Brazil.

Lengo la mazungumzo hayo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya uwili hususan kwenye sekta ya viwanda, biashara, kilimo, nishati utalii pamoja na kutafuta fursa mbalimbali za ushirikiano, uwekezaji na miradi ya pamoja.

Enable Notifications OK No thanks