Rais Samia atua Kenya kwa ziara ya siku mbili
- Amewasili leo asubuhi kwa ziara ya siku mbili nchini humo.
- Anatarajiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti kesho.
- Pia atafanya mazungumzo na Rais Kenyatta na kukutana na wafanyabiashara.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasili nchini Kenya ambapo amepokelewa na viongozi mbalimbali nchini humo katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) tayari kwa kuanza ziara ya kiserikali ya siku mbili.
Akiwa JKIA, Mama Samia amepokelewa na Waziri wa Masuala ya Kigeni Raychelle Omamo, Waziri wa Michezo Dk Amina Mohamed na Kaimu Gavana wa Nairobi Ann Kananu.
Baada ya Rais Samia na ujumbe wake waliokuwa wamevaa barakoa kuwawasili nchini humo, amekutana na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta Ikulu jijini Nairobi ambapo leo watafanya mazungumzo kuhusu mambo mbalimbali baina ya nchi hizo mbili ikiwemo ushirikiano wa kibiashara.
Akiwa Ikulu, Rais Samia amekagua gwaride la kijeshi lililoandaliwa kwa heshima yake kama Amiri Mkuu wa Majeshi ya Tanzania na baadaye kupigiwa mizinga 21.
Kwa mujibu wa televisheni ya Citizen ya nchini humo, baada ya Samia na Kenyatta kufanya mazungumzo, watashiriki dhifa maalum ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na mwenyeji wake.
President Samia Suluhu at State House pic.twitter.com/FhF25aPefJ
— Citizen TV Kenya (@citizentvkenya) May 4, 2021
Siku ya pili ya ziara ya Mama Samia
Katika ziara hiyo, Rais Samia anatarajiwa kufanya shughuli mbalimbali nchini humo ambapo kesho Mei 5, 2021 anatarajiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti, kukutana na wafanyabiashara wa jukwaa la biashara la Kenya na Tanzania.
Atahitimisha ziara yake kwa kushiriki mkutano wa jukwaa la wafanyabiashara wanawake nchini humo na kisha kurejea Tanzania.
Soma zaidi:
Hii ni mara pili kwa Rais Samia kufanya ziara ya kikazi nje ya nchi tangu alipoapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka huu baada ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli.
Mwezi Aprili alitembelea Uganda ambapo alikutana na Rais Yoweri Museveni katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilometa 1,443 kutoka Hoima nchini humo hadi katika bandari Tanga.