TBS: Uivishaji wa ndizi kwa kemikali ya ethylene hauna madhara 

October 16, 2024 11:17 am · Mlelwa Kiwale
Share
Tweet
Copy Link

  • Kemikali hiyo inaruhusiwa kwa matumizi hayo ya kuivisha matunda.
  • Teknolojia hii imepunguza kwa kiasi kikubwa hasara iliyokuwa inajitokeza wakati wa usafirishaji wa matunda.

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka Watanzania kutokuwa na shaka na afya zao baada ya kula ndizi zilizoivishwa kwa kemikali ya ‘ethylene’ kwa kuwa haina madhara.

Hivi karibuni kuliibuka mijadala kuhusu usalama wa afya za Watanzania baada ya baadhi ya wafanyabiashara jijini Dar es Salaam kukiri kutumia kemikali hiyo kuivisha ndizi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa TBS kupitia kwa Meneja wa Uhusiano na Masoko, Gladness Kaseka Oktoba 13, 2024 utaratibu wa kutumia kemikali kuivisha matunda ni wa kawaida na hutumika duniani kote kwa kuwa husaidia kupunguza gharama na upotevu wa chakula.

“TBS inapenda kuufahamisha umma kuwa teknolojia inayotumika kuivisha matunda kwa kutumia kemikali ya ethylene ni utaratibu wa kawaida unaotumika duniani kote na hauna madhara yoyote kiafya. Aidha, kemikali inayotumika ya ethylene imefanyiwa uchunguzi wa kitaalam juu ya usalama wake na inaruhusiwa kwa matumizi hayo ya kuivisha matunda,” imebainisha taarifa na TBS.

TBS imeongeza kuwa teknolojia hiyo imesaidia kupunguza hasara ilivyokuwa ikijitokeza wakati wa usafirishaji wa matunda yalioiva kwa kuwa imewezesha wafanyabiashara kununua/ kusafirisha matunda yaliyokomaa na kuyaivisha kwa wakati mmoja na kwa kiwango sawa.

Aidha, teknolojia hiyo husaidia ndizi hizo kutokuharibika katika kipindi cha muda mrefu zaidi, ikilinganishwa na zile zilizoivishwa kwa njia ya asili ambayo matunda hutoa gesi asilia ya ‘ethylene’ ili kuiva.

Hata hivyo, TBS imesisitiza kuwa inaendelea kulinda usalama na ubora wa bidhaa zote wakati wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks