Ulaji wa matunda na mboga mboga bado bado Tanzania

October 17, 2024 7:14 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Watanzania wanakula gramu 148 za matunda na mboga mboga kwa siku kulinganisha na gramu 400 zinazoshauriwa.
  • WHO yasema kutokula matunda na mboga mboga husababisha magonjwa yasiyoambukiza.

Dar es Salaam. Huenda wadau wa lishe nchini wakatakiwa kuongeza nguvu kuhamasisha ulaji wa matunda na mboga mboga  baada ya ripoti mpya ya hali ya usalama wa chakula Tanzania Bara kubainisha kiwango kidogo cha ulaji wa kundi hilo la chakula nchini.

Kundi la mboga mboga na matunda ni miongoni mwa makundi muhimu ya chakula yanayotakiwa kutumiwa na binadamu kila siku likichanganywa na makundi mengine ya chakula ili kuimarisha Kinga mwili na afya ya mlaji.

Katika kila aina ya tunda au mboga mboga kuna virutubisho ikiwemo vitamini A, B,C, potasiamu, sukari, makapimlo,pamoja na kemikali za mimea.

Licha ya umuhimu huo, ripoti ya hali ya usalama wa chakula Tanzania Bara kwa mwaka 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu (NBS) pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) inabainisha ulaji wa matunda na mboga mboga nchini ni  gramu 148 kwa siku ambao ni chini ya kiwango kinachoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

WHO inashauri ulaji wa  angalau gramu 400 za matunda kwa siku kumlinda mtumiaji na magonjwa ya yasiyoambukiza pamoja na vifo.

Idadi hiyo ni sawa na kusema watanzania hutumika asilimia 37 za matunda kwa siku kulinganisha na idadi inayoshauriwa. 

Kwa upande wa vijijini, ambapo ndipo asilimia kubwa ya mboga mboga na matunda huzalishwa, wastani wa ulaji wa kundi hilo ni gramu 146 kwa siku, wakati mijini ni gramu 147. 

Wakazi wa Dar es Salaam, ndio wanaongoza zaidi katika ulaji wa matunda na mboga mboga kwa wastani wa 162  kwa siku kiasi ambacho huenda kimechochewa na mji huo kuwa kitovu cha biashara kwa watu wengi wa mjini na vijijini.

Kwa mujibu wa chapisho la mtaalam wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dk. Ester Nkuba ameeleza kuwa ni vyema kuyagawa matunda katika milo miwili ili kuongeza uwezekano wa kula kiwango sahihi kinachoshauriwa.

“Katika mlo mmoja unaweza kutumia chungwa moja kubwa au ndizi mbivu moja yenye ukubwa wa kati, tufaa (apple) au embe, au nusu ya parachichi dogo,” amesema Dk Nkuba.  

Athari za kutokula matunda, mboga mboga

WHO  imebainisha kuwa matunda na mboga mboga ni sehemu muhimu za lishe bora, na upungufu wa ulaji wa vyakula hivi unaruhusishwa na afya duni pamoja na kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Inakadiriwa kuwa vifo milioni 3.9 duniani kote mwaka 2017 vilitokana na upungufu wa ulaji wa matunda na mboga mboga.

Enable Notifications OK No thanks