Rais Samia: Mahakama ziwe kimbilio la haki kwa Watanzania
- Awataka watendaji wa Mahakama kujenga imani kwa Watanzania kwa kuwa waadilifu
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Mahakama ya Tanzania kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji haki ili kujenga imani ya wananchi kwa mhimili huo wa dola.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Rais Samia amesema mahakama zinapaswa kuwa kimbilio la kwanza, la mwisho na la kipekee kwa wananchi wanaotafuta haki.
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa Mahakama, hasa zile za mwanzo, kuzingatia zaidi utoaji wa haki badala ya kufungwa na masharti ya kiufundi yanayoweza kuwa kikwazo kwa wananchi.
“Mahakama za mwanzo msifungwe sana na masharti ya kiufundi. Kama ibara ya 107A(2)(i) ya Katiba inavyosema, mahakama itatenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti yanayoweza kuzuia haki kutendeka,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amewataka watendaji wa Mahakama kulinda uadilifu wa majaji na watumishi wa mahakama ili kuimarisha imani ya wananchi na kulinda heshima ya mhimili huo.
Katika kuboresha huduma kwa wananchi, Rais Samia amesisitiza kuwa utoaji wa haki unapaswa kuwa wa kuzingatia mahitaji ya watu (people-centered), akipongeza uanzishwaji wa kituo cha mawasiliano (call center) katika Mahakama.
Hata hivyo, alipokuwa akikabidhi funguo za jengo jipya kwa Jaji Mkuu, Rais Samia amehimiza umuhimu wa kulitunza jengo hilo na miundombinu mingine ya Mahakama, hasa vituo jumuishi vya utoaji haki vilivyojengwa nchi nzima.

“Ujenzi ni jambo moja, lakini utunzaji ni jambo lingine. Ni muhimu majengo haya yatunzwe kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” ameongeza Rais Samia.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel, jengo hilo limegharimu Shilingi bilioni 14.3 na ni la kwanza kwa ukubwa barani Afrika na la sita kwa ukubwa duniani kwa Mahakama Kuu.
Awali, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma, amesema imechukua miaka 104 kwa Mahakama ya Tanzania kupata jengo lake rasmi la makao makuu, akimshukuru Rais Samia kwa hatua hiyo ya kihistoria.
“Mheshimiwa Rais, muda mfupi uliopita umenikabidhi funguo tatu ya dhahabu, fedha na shaba. Hii ni alama ya historia na mwanzo mpya kwa Mahakama ya Tanzania baada ya subira ya miaka 104,” amesema Prof Juma.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa mashauri mahakamani kupitia kampeni za msaada wa kisheria katika mikoa 23, ambapo wasaidizi wa kisheria 2,205 wamepatiwa mafunzo. Aidha, idadi ya taasisi za kisheria imeongezeka kutoka 84 hadi 387 jambo lililosaidia kuongeza kasi ya upatikanaji haki.

Latest