Tanzania yazindua Sera ya Ardhi kukabiliana na migogoro kitaifa, kimataifa

March 17, 2025 7:00 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kupitia upya mfumo wa mabaraza ya ardhi na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vyanzo vya migogoro ya ardhi.

Dar es salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua Sera mpya ya Ardhi inayolenga kufanya maboresho katika sekta hiyo ikiwemo kutatua migogoro ya ardhi ya ndani ya nchi na ya kimataifa ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali ardhi na kuchochea maendeleo,

Rais Samia aliyekuwa akizungumza  katika uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la 2023 uliofanyika leo Machi 17, 2025 jijini Dodoma, amewaambia Watanzania  kuwa sera hiyo imejikita katika kuimarisha haki za umiliki, kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wananchi, wawekezaji, na taasisi za Serikali, pamoja na kuimarisha mahusiano ya mipakani ili kudumisha amani na maendeleo endelevu.

“Tunakwenda kuimarisha uwezo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi…kupitia sera hii tunakwenda kupitia upya mfumo wa mabaraza ya ardhi na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vyanzo vya migogoro ya ardhi” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa kupitia utekelezaji wa Mfumo wa Miundombinu ya Kitaifa wa Taarifa za Kijiografia (National Spatial Data Infrastructure) Serikali itachora ramani ya mpya kuainisha mipaka ya kitaifa na kimataifa ili kutatua migogoro ya ardhi iliyopo ambapo amesisitiza diplomasia itatumika zaidi ili kuhakikisha mchakato huo unazaa matokeo chanya.

“Nadhani huwa mnasikia mara tumebishana na huyu, ziwa limesogea huku , ziwa limezidi huku …tunakwenda sasa kupima tunajua ni changamoto kuna diplomasia ya kutosha lazima itumike” ameongeza Rais Samia.

Uzinduzi wa sera hiyo mpya ya ardhi ni hatua muhimu katika kuhakikisha usimamizi bora wa ardhi na kupunguza migogoro inayotokana na umiliki, matumizi, na mipaka. Picha | Ikulu.

Hata hivyo, katika kuhakikisha migogoro ya ndani ya nchi inatatuliwa, Rais Samia amewaasa watumishi katika sekta ya ardhi kuachana na vitendo vya rushwa kwa kutouza kiwanja kimoja zaidi ya mara moja kwa watu tofauti na kujilimbikizia viwanja wakati wa upimaji wa maeneo.

Kauli ya Rais Samia inakuja wakati ambao migogoro ya ardhi imekuwa ikiripotiwa kwa kiasi kikubwa kwenye jamii ambayo inatajwa kusababishwa na ukosefu wa elimu ya ununuzi wa ardhi pamoja na uwepo wa vitendo vya rushwa kwa wafanyakazi kutoka taasisi zinazohusika na upimaji ardhi.

Rais Samia amesema ili kukabiliana na hilo  Sera mpya inapendekeza matumizi ya mfumo mpya wa Tehama ambao utakomesha vitendo hivyo kwa kuwa utarahisisha utambuzi wa haraka wa umiliki halali wa ardhi katika idara mbalimbali za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Ofisi ya Msajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Uzinduzi wa sera hiyo mpya ya ardhi ni hatua muhimu katika kuhakikisha usimamizi bora wa ardhi na kupunguza migogoro inayotokana na umiliki, matumizi, na mipaka. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks