Zaidi ya wakazi milioni moja, mikoa mitano hatarini kukosa maji Tanzania

January 9, 2024 9:21 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kubainika dawa za kutibu maji zimesalia za siku tatu pekee.
  • Waziri wa Maji atoa saa 12 kwa wakurugenzi wa mamlaka kujitathmini.

Mwanza. Huenda zaidi ya watu milioni moja wanaopata maji kupitia mradi wa maji vijijini unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (Kashwasa) wakakosa maji siku chache zijazo mara baada ya kubainika dawa zinazotumika kutibu maji hayo kusalia za siku tatu pekee.

Wakazi wanaokabiliwa na hatari hiyo ni kutoka mikoa mitano ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Tabora na Singida ambapo kikawaida ni lazima maji yanayopita katika kituo hicho yatibiwe kwanza kabla ya kwenda kutumika na wananchi.

Hayo yamebainika jana Januari 8, 2024 baada ya Waziri wa Maji Juma Aweso kutembelea mradi huo na kubaini dawa zilizopo katika ghala zinafaa kwa muda wa siku tatu pekee tofauti na inavyotakiwa kuwa na angalau akiba ya dawa zinazotosheleza miezi mitatu kabla ya kuagiza shehena nyingine.


Soma zaidi : Punda wanavyorahisisha maisha ya wakazi Iziwa, Mbeya


Pamoja na kutokuwa na dawa za kutosha, Waziri Aweso alibaini mamlaka hiyo kujiendesha kwa hasara licha ya kuwa Serikali iliwekeza zaidi ya Sh900 bilioni kwenye mradi huo ambapo ametoa saa 12 kwa wakurugenzi wa Kashwasa kujitathmini iwapo wanafaa katika nafasi zao.

“Haiwezekani Serikali iwekeze fedha nyingi  kwenye mradi huu zaidi ya Sh900 bilioni zimewekezwa, uje ujiendeshe kwa hasara, hii haikubaliki mnatakiwa mjitathimini na kama mnaona nafasi hiyo imewashinda andikeni barua ya kuachia ngazi,” amesema Aweso.

Aidha, Aweso amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kashwasa Joshua Mgeyekwa kuhakikisha wanatafuta  namna nyingine ya kuendesha mamlaka hiyo badala ya kutegemea kuomba fedha Serikalini.

“Ni aibu kwa uwekezaji mkubwa kama huu, bado mnaomba kulipiwa deni la umeme na kununuliwa dawa za maji, mnashindwaje kuweka mazingira yatakayosaidia kupatikana fedha za kulipia madeni hayo,” amesema Aweso.


Soma zaidi : Utafiti:Zaidi ya watanzania milioni sita hawatumii vyoo


Kashwasa iliundwa mwaka 2008 baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa ziwa Viktoria katika eneo la Ihelele, madhumuni yakiwa kupeleka maji katika maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Shinyanga, Singida na Geita.

Kwa upande mujibu wa Mkurugenzi wa Kashwasa Patrick Nzamba, viwango vya kuzalisha maji katika chanzo hicho umepungua kutoka lita za ujazo milioni 69 mpaka milioni 26 kwa siku, kutokana na ongezeko la matope katika mfumo wa kutibia maji

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW