Rais Samia akemea uuzaji wa karafuu kimagendo Zanzibar
- Asema tatizo hilo ni la muda mrefu na linarudisha nyuma kasi ya maendeleo.
- Atoa wito kwa wananchi kuacha vitendo hivyo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekemea vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara wa karafuu kuiuza nje ya nchi kinyume na utaratibu jambo linaloikosesha Serikali mapato akiwataka kuacha jambo hilo.
Kwa kawaida Serikali kupitia ZSTC hukusanya karafuu kutoka kwa wakulima kisha kuiuza kabla ya kuwapa wakulima fedha zao jambo ambalo linaiingizia Serikali mapato yanayochangia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Rais Samia, aliyekuwa akizungumza baada ya kuzindua jengo la kitega uchumi la Zanzibar State Trade Cooperation (ZSTC) lililopo Pemba, leo Januari 9, 2024 amesema vitendo hivyo vinarudisha nyuma juhudi za Serikali kuleta maendeleo katika visiwa hivyo.
Rais Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaabani kuashiria ufunguzi wa Jengo la ZSTC.Picha|Ikulu.
“Karafuu ndio maendeleo yetu nimesema hapa inachangia asilimia 65.4 …sasa tunapoichepusha tukaiuza nje tunafifisha maendeleo yetu wenyewe wala hatuikomoi Serikali tunajikomoa wenyewe,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kuwa tatizo ni la muda mrefu tangu mwaka 2005/2010 alipokuwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwarai wananchi kuachana na vitendo hivyo na kuiachia Serikali kushughulikia masuala ya masoko.
“Nawasishi sana ndugu zangu suala la magendo hebu tuache na tuiachie Serikali ifanye kazi yake,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:Zaidi ya wakazi milioni moja, mikoa mitano hatarini kukosa maji Tanzania
ZSTC kunufaisha wakulima
Miongoni mwa faida watakazopata wakulima wa zao la karafuu katika visiwa vya Pemba na Unguja baada ya kukamilika kwa jengo la kitega uchumi la ZSTC ni pamoja na uwezo mkubwa kuhifadhi mazao kwa muda mrefu wakati yakisubiri kununuliwa na wateja kwa bei yenye tija zaidi.
“Karafuu zinazouzwa zitahifadhiwa katika maghala safii na ya kisasa…kilichonifurahisha ni kwamba sasa karafuu inanunuliwa kisayansi ile enzi ya kupima unyevu kwa mkono sasa haipo unyevu unapimwa na mashine,” ameongeza Rais Samia.
Latest