Rais Samia akemea tabia ya uharibifu wa barabara
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, pamoja na viongozi wengine wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa Barabara ya Kikanda ya Afrika Mashariki (Arusha Bypass ya kilomita 42.4) katika sherehe zilizofanyika Ngaramtoni Jijini Arusha 22 Julai, 2022.
- Asema vitendo hivyo vinasababisha hasara kwa Serikali.
- Ataka kila mwananchi kutunza miundombinu hiyo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaoharibu miundombinu ya barabara ikiwemo kuchimba mchanga kwa sababu vitendo hivyo vinasababisha hasara kwa Serikali.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza jijini Arusha Julai 22, 2022 wakati wa ufunguzi wa barabara ya Afrika Mashariki (Arusha Bypass) yenye urefu wa kilomita 42.4 amesema kila mwananchi anawajibika kutunza miundombinu ya barabara ili iwanufaishe katika shughuli za usafirishaji.
“Niwaombe sana ndugu zangu kufuata taratibu zilizowekwa ili tuendelee kutunza miundombinu yetu, iendelee kutukuzia uchumi wetu,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi na kueleza kuwa,
“Kumeanza kujitokeza vitendo viovu vya kuharibu miundombinu yetu. Kila siku tunaona Jeshi la Polisi wakizungumzia jinsi ya kutunza barabara zetu kutokutengeneza magari yanayoharibika barabarani kwa sababu wanapofanya hivyo wanamwaga mafuta ambayo yanakwenda kutoboa barabara zetu.”
Lakini suala la kuzidisha uzito wa magari yetu na lenyewe linakwenda kuharibu barabara zetu
Amesema vitendo vingine vinavyoharibu miundombinu ni kuzidisha uzito wa mizigo kwenye magari, kutupa taka kwenye madaraja na kuchimba mchanga.
Aidha, Rais Samia amesema barabara hiyo ya Afrika Mashariki itakuwa kiungo muhimu cha shughuli za biashara na utalii kati ya Kenya na Tanzania.
Barabara ya kimataifa ya Arusha-Holili hadi Taveta, Voi nchini Kenya, awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Sakina- Tengeru yenye urefu wa Kilomita 14.1 iliyojengwa kwa njia mbili kila upande, na barabara ya mchipuo ya jiji la Arusha yenye urefu wa kilomita 42.4.
Akizungumza katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo, Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema barabara hiyo itakuwa na manufaa mengi ikiwemo kuongeza ukaribu wa wananchi, kuimarisha biashara na kurahisisha usafirishaji wa mizigo na bidhaa katika nchi hizo.
“Huo ni utajiri kwa wakulima wa Tanzania na wafanyabiashara wa Kenya na njia ya kumaliza umasikini katika nchi zetu,” amesema Rais Kenyatta huku akieleza kuwa miundombinu ndiyo msingi wa maendeleo.
Zinazohusiana:
- VTS: Vifaa vya kudhibiti ajali vinavyoogopwa na madereva waluwalu
- Serikali yaangazia daladala, mabasi ya mikoani kuongeza mapato kielektroniki
Kwa mujibu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, Sh197.45 bilioni zimetumika kugharamia ujenzi huo huku Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania ndizo zilizogharamia ujenzi huo uliofanyika kwa kipindi cha miezi 46.
Amesema barabara hiyoi ni sehemu ya barabara kuu inayounganisha ukanda wa kaskazini (northern corridor) hadi mpaka wa kaskazini wa Tanzania na Kenya kule Holili-Taveta na kuishia Voi kilomita 160 kutoka mji wa Mombasa.
“Barabara hii baada ya kuboreshwa imepunguza kwa kiwango kikubwa muda wa usafiri kati ya bandari za Tanga na Mombasa, kwenda na kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma na maeneo mengine ya nchi yetu na Nchi majirani,” amesema Prof Mbarawa.
Pia barabara hiyo ni kiunganishi muhimu na sehemu ya ushoroba wa kaskazini (Great North Road) ambao pia hujulikana kama ushoroba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki namba 5 ambayo inatoka Cape Town Afrika ya Kusini hadi Cairo Misri kupitia Zambia na kuingia kwenye mji wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Latest