Rais Samia aziagiza Takukuru, Zaeca kufuatilia na kuichukulia hatua miradi yenye kasoro
- Asema vitendo vya rushwa havivumiliki.
- Viongozi waagizwa kusimamia fedha za miradi zinzotolewa na Serikali.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufuatilia miradi ya maendeleo iliyobainika kuwa na dosari na kuwachukulia hatua wahusika.
Rais Samia ameyasema hayo kwenye hafla ya Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana iliyofanyika katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera leo (14, Oktoba 2022).
Rais Samia amesema vitendo vya rushwa havivumiliki na mapambano ya dhidi ya vitendo hivyo ni lazima yaendelee.
“Hatuwezi kuvumilia uzembe na kutokuwajibika kunakosababishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi,” amesema Rais Samia.
Sambamba na hilo taasisi hizo zenye kupambana na rushwa nchini zimeagizwa kuwachukulia hatua wasimamizi wa miradi iliyobainika kuwa na ufujaji, wizi, matumizi mabaya ya fedha, pamoja na rushwa.
Agizo hilo la Rais Samia limekuja mara baada ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwenye miradi mbalimbali nchini hali inayopelekea miradi hiyo kutofikia viwango vinavyotakiwa.
“Kama Taifa bado tunaendelea kutafunwa na vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo ni adui mkubwa wa maendeleo,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:
-
Rais Samia aeleza mambo 3 kumuenzi Mwalimu Nyerere
-
Rais Samia: Wakuu wa wilaya fanyeni kazi msisubiri ‘mkeka’
Viongozi simamieni fedha za miradi
Rais Samia amewataka viongozi na watendaji wahakikishe wanasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazoelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tunafanya hivyo tukiamini viongozi na watendaji wa ngazi zote watahakikisha wanasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazopelekwa kwao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” ameongea Rais Samia.
Rais Samia pia amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wasiojali na kuhurumia wananchi kwa kuwapa miradi wakandarasi wasio na uwezo na kusababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo.
“Inasikitisha kuona kwamba kuna watu wasiojali na wasio na huruma kwa wananchi kwa kuwapa miradi wakandarasi wasio na uwezo, watu waliotawaliwa na rushwa, wezi na wengine ni wazembe wanaosababisha miradi kutokukamilika,” amesema Rais Samia
Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2022 zilikuwa na ujumbe maalumu wa sensa chini ya kauli mbiu isemayo ‘Sensa ni Msingi wa Maendeleo Shiriki Kuhesabiwa Tuyafikie Maendeleo ya Taifa’.
Mbio hizo zilizinduliwa Aprili 2, 2022 ambapo miradi ya maendeleo 1,293 iliyogharimu Sh6508 bilioni ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Latest
