Rais Samia akemea matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana Tabora
- Awataka kuelekeza nguvu zao katika shughuli za uzalishaji ili wainuke kiuchumi.
- Auagiza uongozi wa mkoa, wilaya na CCM kuwasimamia vijana.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka vijana wa Nzega mkoani Tabora, kutumia vyema miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo kujiimarisha kiuchumi na kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Samora, wilayani Nzega leo Octoba 17, 2023 amewaambia vijana kusitisha mara moja matumizi ya madawa ya kulevya huku akiuagiza uongozi wa Mkoa wa Tabora pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulisimamia suala hilo.
Nizungumze na ninyi vijana wangu, hii safari na huu uraibu unaoingia hauwafai na hautawapeleka pazuri, naomba sana Serikali ya mkoa, wilaya, na CCM simamieni hili…
… vijana wetu waende kwenye maeneo ya kuzalisha, wasiingie kwenye majanga, hii si desturi, mila na historia ya Nzega, niombe sana vijana nendeni kwenye maendeleo, msiende kujibomoa,” amesisitiza Rais Samia mkoani Tabora.
Soma zaidi : Kasi ya maendeleo mkoani Singida yamkwaza Rais Samia
Awali Rais Samia alibainisha kuwa miongoni mwa miradi inayotekelezwa mkoani Tabora ili kutengeneza fursa za kiuchumi kwa vijana ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya mafunzo stadi Veta, ujenzi wa viwanda vya kati, pamoja na mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT).
“Serikali yenu inatumia pesa nyingi kujenga vyuo ivya kuwafundisha, kuweka miradi ya umwagiliaji ili kilimo kikue, kuleta mbolea na kuweka ruzuku ya mbolea ili vijana mjiingize huko, mfanye kazi na mpate mapato yenu ya halali,” ameongeza Rais Samia.
Sambamba na hilo, Rais Samia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wasichana wa Nzega na Mkoa wa Tabora kwa ujumla, kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao kielimu kwa kuwa Serikali imerahisisha upatikanaji wa elimu kwa kujenga shule, kutoa elimu bila ada pamoja na kuboresha Sera za elimu ambapo kwa sasa wasichana waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali wanaruhusiwa kuendelea na masomo.
Latest
