Kasi ya maendeleo mkoani Singida yamkwaza Rais Samia

October 16, 2023 4:12 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema miaka 60 ni mingi kwa mkoa huo kuwa na kiwango kidogo cha maendeleo.
  • Mchango wake kwa pato la Taifa ni chini ya asilimia mbili
  • Asisitiza mabadiliko ya tabia ili kuleta maendeleo


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema haridhishwi na kasi ya maendeleo ya kiuchumi mkoani Singida kwa kuwa bado maendeleo yaliyopo hayaendani na umri wa miaka 60 ulionao mkoa huo huku akiwataka wakazi wake kutumia vyema fursa zilizopo kukuza uchumi.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Mkoa wa Singida, leo Oktoba 16, 2023, amesema haiwezekani kwa mkoa wenye umri huo kuchangia chini ya asilimia mbili kwenye  pato la Taifa huku ukisalia kuwa miongoni mwa mikoa masikini zaidi Tanzania.

“Ukipanga mikoa masikini zaidi nchini Singida ipo, lakini fursa alizotuumbia Mungu ni nyingi mno, kakaeni muangalie, mjitathmini na mje na mpango tutakaoweza kuwasaidia muende mbele zaidi..

“…Imani yangu ni kwamba tungekuwa mbali zaidi kuliko hapa, miaka 60 ni mingi sana,” amesema Rais Samia.


Soma zaidi:BOT yatoa kanuni mpya kwa maduka ya kubadili fedha za kigeni Tanzania


Kwa mujibu wa Rais Samia bado wakazi wa mkoa huo hawajazitumia vyema fursa za kiuchumi zinazowazunguka ikiwemo machimbo ya dhahabu, uzalishaji wa zao la alizeti kwa ajili ya mafuta na urinaji asali.

Kitabu cha takwimu za msingi za Tanzania mwaka 2022 (Tanzania in Figures ) kinautaja mkoa wa Singida kuwa miongoni mwa mikoa 10 yenye wakazi wenye kipato kidogo zaidi ambacho kipo chini ya wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja nchini Tanzania cha Sh2.8 milioni.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Mkoa, Wabunge pamoja na Chama wakikata  keki wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya mkoa wa Singida yaliyofanyika katika uwanja wa Bombadia Singida.Picha|Ikulu.

Mkoa huo umeshika nafasi ya tatu, ambapo wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kwa wakazi wake ni Sh1.5 milioni kwa mwaka kiwango ambacho kimeendelea kusalia chini ya wastani kwa miaka mitano mfululizo.

Hata hivyo, mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na ukame na ukosefu wa mvua katika misimu mingi jambo linalokwamisha baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo.

Kufuatia changamoto hiyo, Rais Samia amesema Serikali yake ipo tayari kuusaidia mkoa huo ili kuhakikisha unakua zaidi kiuchumi kwa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa mkoa huo una ardhi ya kutosha kufanikisha hilo.

“Kakaeni kwenye vikao vyenu mjiulize kama mmefanikiwa sawa, lakini mkiona bado je mna mipango gani ya baadae muilete Serikalini tuweke nguvu zetu na Singida ipae kimaendeleo,” ameongeza Rais Samia.

Tabia za viongozi bado kikwazo

Aidha,miongoni mwa mambo yaliyomuudhi Rais Samia ni pamoja na  kutofunguliwa kwa vituo 15 vya afya kwa wakati licha ya kukamilika kwake, jambo lililowakosesha wakazi wa maeneo hayo huduma muhimu ya afya wakati Serikali ilishatumia muda na fedha kugharamia ujenzi huo.

“Tuangalie tatizo hapa ni nini badala ya mabadiliko ya tabia ya nchi sasa tuelekee kwenye mabadiliko ya tabia watu…tuendelee kubadilika ili tuweze kutumia fursa zilizopo na Singida iende mbele,” amesema Rais Samia.

Rais Samia anatarajia kumaliza ziara yake mkoani Singida kesho ambapo anatarajiwa kuzindua mradi wa maji ziwa Viktoria, kutembelea jimbo la Iramba Magharibi na kuanza ziara ya kikazi mkoani Tabora.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW