Rais Samia afanya mabadiliko makatibu tawala wa mikoa

July 28, 2022 6:40 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Makatibu tawala tisa wahamishwa vituo vya kazi.
  • Kumi wapya wateuliwa.
  • Wateule hao wataapishwa Agosti 1, ikulu Dodoma.

Dar es Salaam. Rais  Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa makatibu tawala wa mikoa wapya saba na kuwahamisha vituo vya kazi 10 na wengine tisa kubakia kwenye vituo vyao vya awali.

Taarifa ya Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo Julai 29, inasema uapisho wa wateule hao utafanyika Agosti mosi, ikulu Chamwino Dodoma.

Hii inakuwa mara ya nane Rais Samia kufanya teuzi mbalimbali ndani ya mwezi mmoja, ambapo mwanzoni mwa mwezi wa saba alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari TPA, Eric Hamisi na kumteua Mkeli Mbosa kushika nafasi hiyo.


Makatibu tawala za mikoa wapya

Katika taarifa hiyo vigogo walioingizwa kwenye mkeka wa makatibu tawala wapya ni pamoja na  Kamishna Dk Mussa Ali Mussa aliyeteuliwa kuwa  katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro huku Profesa Godins Walter Kalyarara akiteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita.

Awali Prof. Klyara alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara.

Mhandisi Leonard Robert Masanja ameteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ambapo awali alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Dar es Salaam.

Rais Samia pia amemteua Toba Alnason Nguvila kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera. Awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera.

Kigogo mwingine aliyeingia kwenye mkeka wa makatibu tawala wapya ni Elikana Mayuganya Balandya aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza. Awali alikuwa Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango.

Wengine ni Profesa Siza Donald Tumbo aliyeteuliwa  kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo. 

“Dk John Rogath Mboya ameteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora. Alikuwa Kamishna wa Idara ya Bajeti katika Wizara ya Fedha na Mipango,” imeeleza taarifa ya Zuhura.


soma zaidi


Waliohamishwa vituo vya kazi

Mkeka huo pia umeainisha majina ya 10 ya makatibu tawala waliohamishwa vituo vyao vya kazi. Makatibu hao ni pamoja na Missile Albano Musa aliyehamishwa kutoka Mkoa wa Songwe na kupelekwa Arusha. 

Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Rehema Seif Madenge ameteuliwa kuwa  Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam akichukua nafasi nafasi ya Hassan Abbas Rugwa ambaye amehamishiwa Mkoa wa Katavi.

Ngusa Dismas Samike amehamishwa Mkoa Lindi akitokea Mwanza huku Msalika Robert Makungu amehamishwa Mara awali akitokea Mkoa wa Tabora.

Msovera Albert Gabriel kutoka Mara anaenda kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mkoa wa Kigoma. Huku Rodrick Lazaro Mpogolo amehamishiwa Mbeya akitoka Katavi.

Zuwena Omari Jiri, amehamishiwa Mkoa wa Pwani akitokea Shinyanga. Happiness William Seneda, amepelekwa Mkoa wa Songwe akitokea Iringa na Rashid Kassim Mchata wa Rukwa amepelekwa Mkoa wa Kigoma.


Makatibu tawala ambao hawajaguswa na mabadiliko hayo

Katika mkeka huo kuna orodha ya makatibu tawala ambao panga pangua ya Rais Samia haikuwagusa akiwemo Dk Fatuma Ramadhan Mganga wa Mkoa wa Dodoma na Karolina Albert Mthapula wa Manyara.

Wengine ni pamoja na Abdallah Mohamed Malela wa Mkoa wa Mtwara

Judica Haikale Omary (Njombe), Willy Lugahyulula Machumu (Kilimanjaro), Steven Mashauri Ndaki (Ruvuma), Dorothy Aidan Mwaluko (Singida), Prisca Joseph Kayombo (Simiyu) na Pili Hassan Mnyema wa Tanga.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW