Rais Samia ateua wakuu wa wilaya wakiwemo vigogo wa Tanapa, Ngorongoro
- Ni katika pangapangua ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala.
- Bosi wa Tanapa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe aikichukua nafasi ya Jokate.
- Wengine waliohamishwa ni Sixtus Mapunda ambaye anachukua nafasi ya Mobhare Matinyi aliyeteuliwa kuwa msemaji mkuu wa Serikali.

Dar es Salaam. Bado hakijaeleweka! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko mengine kwa kuteua baadhi ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wapya wakiwemo vigogo wa juu wa mashirika ya uhifadhi nchini.
Mabadiliko hayo yanakuja ikiwa ni siku 92 tangu afanye uteuzi wa mwisho wa viongozi wa nafasi hiyo, ikiwa ni muendelezo wa panga pangua ndani ya Serikali yake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus amesema Rais Samia amemteua William Mwakilema aliyekuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
Mwakilema anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jokate Mwegelo ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Kujaza nafasi ya bosi huyo, Rais Samia amemteua Musa Kuji kuwa Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa.
Sanjari na bosi huyo wa Tanapa, Rais Samia amemteua pia Elibariki Bajuta, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora.
Soma zaidi : Rais Samia apangua vigogo TTCL, Tanesco, vilio vya umeme vikiendelea Tanzania
Bajuta anachukua nafasi ya Kenan Kihongosi ambaye amehamishwa kuwa mkuu wa wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Kihongosi anachukua nafasi ya Fakii Lulandala ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Viongozi hawa ni kama wamebadilishana nafasi ya uongozi kwa kuwa Lulandala kwa sasa anashika nafasi ambayo Kihongosi alikuwa akiihudumu hadi Mei 23, 2023 kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo.
Kihongosi alihudumu nafasi ya Katibu Mkuu wa UVCCM kuanzia Juni 22, 2021 baada ya Kamati Kuu ya (CCM) kumteua katika nafasi hiyo akichukua nafasi ya Raymond Mwangala ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro .
Wengine walioteuliwa
Yunus amesema Rais Samia amemhamisha Sixtus Mapunda kutoka Wilaya ya Sumbawanga kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, akichukua nafasi ya Mobhare Matinyi aliyeteuliwa jana kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Soma zaidi : Rais Samia amteua Mobhare Matinyi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali
Mwingine katika uteuzi huo uliotangazwa leo (Oktoba 3, 2023) ni Nyakia Chirukile ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga akichukua nafasi ya Mapunda aliyehamishiwa Wilaya ya Temeke. Awali Chirukile alikuwa Katibu Tawala wa Ngorongoro.
Sambamba na hilo Rais Samia amemfuta kazi Halfan Magani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe na kumteua Goodluck Mwangomango kushika wadhifa huo.
Wengine ni Said Majaliwa aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tanga Mjini, Faraja Paschal Msigwa kuwa Mkurugenzi wa Kilindi Mkoani Tanga, Naima Bakari Chondo kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida Mjini, Shamim Adam Sadiq kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa na Hamza Hussein Hamza kuwa Katibu Tawala Wilaya ya Ngorongoro.
Taarifa hiyo ya uteuzi iliyotoka usiku wa leo imebainisha kuwa Lameck Karanga Ng’ang’a ameteuliwa kuwa katibu tawala wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Latest