Rais Samia aahidi kuendeleza ushirikiano na Namibia, akimpongeza Rais Netumbo

March 21, 2025 4:38 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema Rais Netumbo amekuwa kielelezo kwa mabinti wa Namibia na Afrika kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
  • Milango ya Tanzania ipo wazi kuendelea kushirikiana na Namibia.

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Netumbo Nandi -Ndaitwah kwa kuapishwa kuwa Rais wa Namibia  huku akihimiza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Netumbo alitangazwa kuwa mshindi wa kinyanganyiro wa urais wa nchi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Decemba, 2024 akipata asilimia 57 ya kura na kumuacha nyuma mpinzani wake Panduleni Itula aliyepata asilimia 26 ya kura

Kwa ushindi huo Netumbo ameapishwa hii leo Machi 21, 2025 kuwa Rais wa tano wa nchi hiyo akitarajiwa kuiongoza kwa miaka mitano ijayo akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Nangolo Mbumba aliyeongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee.

Mbumba alishika nafasi hiyo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hage Gottfried Geingob kilichotokea  Februari 4, 2024.

Akihutubia wahudhuriaji wa sherehe za uapisho huo zilizofanyika leo Machi 21, 2025  Rais Samia amempongeza Rais Netumbo kwa kuwa kioo kwa wasichana na wanawake wa Namibia na Afrika kwa ujumla.

“Nakupongeza kwa kuandika historia mpya, lakini pia kwa kuweka viwango vya juu kwa Afrika na kwa mtoto wa kike wa Namibia, ushindi wako wa kishindo ni fahari kubwa kwa bara letu lakini pia kwa watu wa Tanzania nyumbani kwako katika sehemu kubwa ya miaka yako ya awali,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan(kushoto) akimpongeza Rais Mteule wa Jamhuri ya Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah mara baada ya kuhutubia hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya nchi hiyo, Picha|Ikulu.

Pamoja na hayo, Rais Samia amemuahidi Rais Natumbo ushirikiano katika masuala yote ya kiungozi pamoja na kuimarisha mahusiano ya kindugu yaliyodumu kwa miongo mingi tangu harakati za kudai uhuru.

“Tunakutakia kila la heri katika jukumu hili jipya, tunakuhakikishia pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Namibia kwamba Serikali yetu imejizatiti kuendeleza urafiki wa kweli na ushirikiano wa kudumu uliopo kati ya nchi zetu…

…Milango yetu ipo wazi kwa mashauriano, mijadala, na hata kubadilishana uzoefu, kwa kuwa tunaamini katika wajibu wetu wa kimaadili wa kuwawezesha na kuwaendeleza kizazi kijacho cha Afrika.

Kwa upande wake Rais Netumbo amesema kuwa kuingia kwake madarakani ni kielelezo tosha kuwa mwanamke anaweza kushika nyadhifa yoyote ya uongozi akihimiza kuongeza nguvu zaidi katika ukombozi wa mwanamke barani Afrika.

“Sikuchaguliwa kwa sababu mimi ni mwanamke, bali kwa sifa na uwezo, hiyo ni kusema, wanawake hatupaswi kuomba kuchaguliwa kwenye nyadhifa za uwajibikaji kwa sababu tu sisi ni wanawake, bali kwa sababu tuna uwezo wa kuwa wanachama wenye sifa stahili. Na hilo ndilo jambo la msingi,” amesema Netumbo.

Pamoja na hayo kiongozi huyo ameahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikumba nchi hiyo ikiwemo rushwa, mabadiliko ya tabia ya nchi na kuinua kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks