Rais Samia kufanya ziara ya kikazi Namibia
- Pamoja na kushuhudia kuapishwa kwa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais Samia atalihutubia Taifa hilo.
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika Jamhuri ya Namibia leo Machi 21, 2025 kuhudhuria sherehe za uapisho wa Rais mteule wa nchi hiyo Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Taarifa ya Sharifa Nyanga, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu iliyotolewa Machi 20, 2025 inabainisha kuwa pamoja na kuhudhuria uapisho huo Rias Samia atahutubia wahudhuriaji wa hafla hiyo.
“Rais Samia amealikwa kama mgeni Rasmi na anatarajia kuhutubia kwenye sherehe hizo za uapisho zitakazofanyika sambamba na maadhimisho ya Miaka 35 ya Uhuru wa Namibia.” imesema taarifa ya Sharifa.
Kuapishwa kwa Rais Nemtumbo kunafanya idadi ya Marais wanawake barani Afrika kuwa wawili akiwemo Rais Samia jambo linaloendelea kuchochea usawa wa kijinsia barani humo.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais Netumbo (72) aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano, Waziri wa Mazingira na Utalii, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia na nafasi ya Naibu Waziri Mkuu aliyohitimisha nayo kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais.
Ushindi wake unaendeleza utawala wa miaka 34 wa chama cha SWAPO madarakani, tangu Namibia ilipopata uhuru kutoka kwa Afrika kusini mwaka 1990.
Mbali na Rais Samia, sherehe hizo zitahudhuriwa pia na wakuu wa nchi nyingine 10 barani Afrika, Makamu wa Rais watatu, wakuu wa nchi wastaafu saba pamoja na mawaziri wakuu wawili.
Pamoja na kuwa miongoni mwa wahudhuriaji, ushiriki wa Rais Samia katika sherehe hizo kunaendeleza mahusiano chanya ya kindugu kati ya Tanzania na Namibia yaliyodumu kwa miongo yakiasisiwa na Hayati Julius Nyerere na Hayati Sam Nujoma kipindi cha harakati za ukombozi wa nchi hizo.
Mahusiano haya yameendelea kukuzwa na kulelewa na viongozi wote wakuu waliowafuatia katika nyanja mbali mbali.
Mbali na kuhudhuria sherehe hizo Rais Dkt. Samia atapata fursa ya kusalimiana na mwenyeji wake na kufanya mazungumzo ya kukuza na kuimarisha mahusiano.
Latest



