Rais Samia aagiza ‘boom’ kuwa Sh10,000 kwa siku Tanzania

February 11, 2023 1:28 pm · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya wanafunzi kueleza changamoto  za mikopo ikiwemo ucheleweshaji ‘boom’ vyuoni
  • Ongezeko hilo iwapo litatekelezwa mapema litapunguza maumivu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuongeza pesa ya kujikimu kwa wanafunzi wanaopata mkopo wa elimu ya juu hadi Sh10,000 kwa siku kutoka Sh8,500 ya sasa, hatua itakayopunguza makali ya maisha.

Ongezeko hilo iwapo litatekelezwa mapema litapunguza maumivu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakilalamika kuwa kiwango cha fedha za kujikimu maarufu kama ‘Boom’ kinachotolewa kwa sasa hakikidhi mahitaji kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma. 

Rais Samia ametoa agizo hilo leo Februari 11, 2023 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) na lile la upande wa Zanzibar (Zahilfe). 

Hatua hiyo imekuja baada ya wawakilishi wa shirikisho kutoka vyuo mbalimbali nchini kuwasilisha changamoto zao ikiwemo ya ucheleweshaji wa mikopo vyuoni hivyo kusababisha ugumu wa maisha.

Katika kujibu baadhi ya maswali na changamoto zilizotolewa na wanafunzi hao, Rais Samia ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutazama kiwango hicho cha kujikimu vyuoni ili kianze kuwa Sh10,000 kwa siku.

“Suala la boom kwa sababu naambiwa boom ikimalizika mnafanyaje mnapiga ndefu sijui mnafanyaje…unajipanga ule mara moja kwa siku, sasa Waziri wa Elimu nenda kaangalie tutaanza na Sh10,000,” Rais Samia amesema.

Agizo hilo la kuongezwa kiasi hicho litafanya wanafunzi hao kuweka kibindoni Sh1,500 sawa na ongezeko la asilimia 18.

Hata hivyo, Mwongozo wa utoaji mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2021/2022 umebainisha kuwa mwanafunzi atapata kiasi cha Sh10,000 kwa siku wakati wa mafunzo chuoni kwa ajili ya chakula na malazi. 

Baadhi ya wanafunzi wameiambia Nukta Habari kuwa bado wanapata Sh8,500 kwa siku badala ya Sh10,000 iliyopo kwenye mwongozo.

Abdushakur Mrisho, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino mkoani Mwanza amesema akiwa bado mnufaika wa mkopo hadi sasa anapokea kiwango cha Sh8,500.

“Maoni yangu ni kuwa suala hili lisiishie kisiasa endapo litatekelezwa litakuwa jambo bora kwetu wanafunzi,” amesema Mrisho.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW