Kimeumana: Mikopo ya halmashauri kuanza kutolewa benki
- Sh88 bilioni zayeyuka kwa vikundi hewa.
- Madiwani watajwa upigaji fedha za mikopo hiyo.
- Samia ashauri mikopo itolewe benki badala ya halmashauri kuanzia mwaka ujao wa fedha.
Dar es Salaam. Huenda utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ikapata sura mpya kuanzia mwaka ujao wa fedha mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka uwekwe mfumo mpya wa utoaji mikopo hiyo.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/22 kubainisha kuwa Sh88 bilioni zilizotolewa kama mikopo hazikurejeshwa na hazitarejeshwa.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akipokea ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam leo Machi 29, 2023 amewaambia Watanzania kuwa jambo hilo linasababishwa na utaratibu mbovu wa utoaji mikopo hiyo na ufuatiliaji hafifu.
“Bilioni 88 imekwenda haijakusanywa na haikusanyiki, na hii ni kwa sababu vikundi vinavyopewa ni hewa, uadilifu kwa madiwani ni hewa na pili wanaopewa wanaona wamepewa na madiwani wao, hawaoni umuhimu wa kurejesha kwa hiyo tunahitaji marekebisho makubwa,” amesema Rais Samia.
Marekebisho yanayotajwa na Rais Samia yanahusu kubadili mfumo wa utoaji mikopo hiyo kutoka halmashauri mpaka katika benki ambayo itakuwa imeteuliwa na Serikali kusimamia jambo hilo.
“Njia itayotufaa ni ya kutumia mfumo wa benki, tupige hesabu ya asilimia 10 inayohitajika katika halmashauri husika kisha ikakae benki, wanaohitaji mikopo wataenda benki, kwa sababu benki uwe unataka au hutaki lazima utarejesha,” amesisitiza Rais Samia.
Zinazohusiana:
Rais Samia amesema mfumo huo utasaidia pesa kurejeshwa kwa wakati na kupunguza urasimu uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa za Mwaka 2019, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakuwa na wajibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Katika asilimia hizo10, asilimia nne ya fedha ni kwa ajili ya wanawake, asilimia nne kwa ajili ya vijana na asilimia mbili ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/23 Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi ilitenga jumla ya Sh79.97 bilioni kwa ajili ya mikopo ya maendeleo kwa vijana, wanawake na walemavu.
“Kati ya fedha hizo, Sh30.39 bilioni ni kwa ajili ya vikundi vya wanawake, Sh30.39 ni kwa ajili ya vikundi vya vijana na Sh15.19 bilioni ni kwa ajili ya vikundi vya watu wenye ulemavu,” unafafanua mchanganuo wa bajeti hiyo.
Latest
