Rais Magufuli asema ‘flyovers’ nyingine zaja Dar

Msafara wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli,ukipita katika daraja la juu la mhandisi Mfugale (flyover Mfugale) Picha|Michuzi blog.
- Rais Magufuli asema zabuni ya ujenzi wa daraja jingine la juu la Chang’ombe imeshatangazwa.
- Aagiza flyover ya Mfugale ifungwe kamera za usalama ili kuongeza usalama katika eneo hilo.
Dar es salaam. Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la juu lililopo katika makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere (Mfugale Flyover), Rais John Magufuli amesema Serikali imeanza mchakato wa kujenga mengine ya Chang’ombe na Uhasibu (Machinjioni).
Taarifa za kuanza mchakato wa ujenzi wa madaraja hayo zinakuja wakati mkandarasi wa kampuni ya CCECC akiendelea na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Mandela ambayo inatarajia kuwa na ngazi tatu.
Rais Magufuli aliyekuwa akijibu ombi la Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum juu kujengwa madaraja mengine ya juu wakati wa uzinduzi wa daraja Mfugale Flover leo (Septemba 27, 2018), amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara na madaraja ya juu mengi zaidi yatakayopunguza foleni.
Katika uboreshaji huo wa miundombinu, Rais Maguguli amesema kwa sasa imeshatangazwa zabuni ya kujengwa barabara kutoka Mbagala, Gerezani, Kivukoni, Changombe hadi Magomeni zenye urefu wa jumla ya kilomita 21 kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
“Pia, itajengwa ‘flyover’ (daraja la juu) Chang’ombe na Mhasibu House (Machinjioni) napo panajengwa flyover na tender (zabuni) imeshatangazwa kwa hiyo Sheikh Mkuu hii siyo flyover ya kwanza zinakuja zingine,” amesema Rais Magufuli.
Dk Magufuli amesema madaraja hayo yatakayojengwa jijini hapa na lile la Ubungo lilitakalogharimu Sh247 bilioni yatasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza foleni ambayo kwa mwaka inaligharimu taifa takriban Sh400 bilioni.
“Mfugale flyover imegharimu Sh106 bilioni Ubungo itagharimu Sh247 bilioni kwa hiyo kama haka ni kamfugale lile ni limfugale,” amesema Rais Dkt John Magufuli na kuwaacha watu wakicheka.
Zinazohusiana: Ahueni ya foleni: Magari yaruhusiwa kuanza kupita ‘Flyover’ ya Tazara Dar
Wakati huo huo Rais Magufuli ameagiza daraja lote la Mfugale lifungwe kamera za usalama mara moja ili kuongeza usalama katika eneo hilo ikiwemo kubaini wanaosababisha ajali na kutoweka.
“Hatutaki kuona watu wanakufa hapo tunataka tuwaone kwa hiyo kazi ya kufunga kamera lifanyike mara moja na madaraja makubwa yote flyover ziwekewe ‘option’ ya kufungwa kamera ili akitokea mtu amelewa na kasababisa ajali ajulikane ni nani,” amesema Rais Magufuli.
Pamoja na kuishukuru Serikali ya Japan kwa ujenzi wa mradi huo uliojengwa ndani ya muda na kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction Co ltd, Rais Magufuli ameiomba serikali ya nchi hiyo kukamilisha ahadi yake ya kujenga Flyover nyingine ya Gerezani na barabara ya Morocco hadi Mwenge yenye urefu wa kilomita 4.1.

Rais John Magufuli akipeana mikono na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Elias Kwandikwa mbele ya Balozi wa Japan Masaharu Yoshinda. Picha| Michuzi blog.
Latest