Profesa Mahalu: Mkapa alikuwa kiongozi aliyesimamia haki

July 27, 2020 6:30 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Amemuelezea kama kiongozi aliyetaka usawa kwa watu wote na hakupenda kupindishwa kwa haki. 
  • Amkumbuka alivyomsaidia kujinasua katika kesi ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. 

Mwanza. Wakati Watanzania wakiendelea kuaga mwili wa Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, watu mbalimbali wameendelea kuelezea jinsi walivyomfahamu kiongozi huyo hasa uthabiti wake wa kusimamia haki. 

Mzee Mkapa alifariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa Julai 24, 2020 hospitalini jijini Dar es Salaam na atazikwa katika kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Julai 29 mwaka huu.

Msimamo thabiti na kusimamia haki kwa wananchi wanyonge ni moja kati ya mambo makuu ambayo atakumbukwa nayo hayati Mkapa.

Hivyo ndivyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut), Profesa Costa Mahalu alivyomfahamu Mzee Mkapa siku za uhai wake. 

“Huyu ndiye rais tuliyekuwa naye ambaye alikuwa na mitazamo ya kila mmoja kujitegemea kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kukaribisha wawekezaji kutoka nje ya nchi, rais ambaye hakupenda mtu aonewe na alichukia rushwa,” amesema Profesa Mahalu wakati akizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki jijini Mwanza. 

Huku akibubujikwa na machozi, Profesa Mahalu amesema Mkapa alikuwa mfano bora kwa uongozi wake na amekuwa akikutana naye mara kwa mara kujadiliana mambo mengi hususan katika kuimarisha uchumi wa nchi.


Zinazohusiana:


Amkumbuka alivyosaidiwa na Mzee Mkapa

Profesa Mahalu pia anakumbuka kiongozi huyo alivyomsaidia wakati Serikali ilipomfikisha mahakamani mwaka 2012 kuhusiana na mkataba wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Lakini baadaye Prof Mahalu alishinda kesi kutokana na kukosekana kwa ushahidi uliokamilika kwa kila shtaka lilikuwa likimkabili la ubadhirifu wa mali za umma. 

“Kwa kweli kifo chake kimeniumiza sana kwani alikuwa kaka yangu wa karibu na rafiki yangu, nitamkumbuka sana,” amesema  Profesa Mahalu huku akibubujikwa na machozi.

Atamkumbuka katika uongozi wake wa kukabiliana na rushwa,  kuondoa uchumi tegemezi na kujenga miundombinu mbalimbali kwa ajili ya utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu. 

Msomi huyo amesema mwaka 1988 alikutana na Mzee Mkapa Geneva, Uswis wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambapo alipigania sana ukombozi wa Afrika ili nchi za bara hilo zijitawala zenyewe.

“Nilifurahi sana kushikana mkono na kiongozi huyo na toka siku hiyo nikawa namfuatilia kwa umakini mambo mengi  hususani katika mitizamo yake ya kukemea ubeberu wa Afrika Magharibi,”amesema.  

Baada ya Hayati Mkapa kushinda kiti cha urais mwaka 1995 alimteua Profesa Mahalu kuwa balozi wa Tanzania nchini Italia.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

Nukta TV