Potofu: Mtoto hapotezi urijali kwa kudondokewa na kitovu

October 4, 2025 3:07 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni utamaduni uliotumika na wazee wa zamani kumfanya mama awe makini na mtoto anapojifungua.

Dar es Salaam. Huenda ukawa ni miongoni mwa watu waliowahi kusikia au kuaminishwa dhana ya kwamba mtoto wa kiume mara baada ya kuzaliwa akiangukiwa na kitovu chake sehemu za siri hupoteza uwezo wa kuzalisha anapokuwa mkubwa. 

Dhana hii imeishi miongoni mwa watu kwa muda mrefu kiasi cha mama anapojifungua kuwa makini kwa kiasi cha kumlaza mtoto kwa namna tofauti ambazo hata muda wa kitovu chake kukatika unapofika hakiangukii katika sehemu za siri.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na NuktaFakti kwa kuzungumza na wataalamu wa afya na kupitia majarida mbalimbali ya sayansi ya tiba unabainisha kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha dhana hiyo bali ni imani zitokanazo na tamaduni zilizorithishwa kutoka kwa wazee wa zamani. Kwa ufupi taarifa hiyo ni potoshi. 

Ukweli ni huu

Daktari wa afya ya uzazi, Joseph Mapunda ameiambia NuktaFakti kuwa hakuna uhusiano wowote wa kisayansi kati ya kuanguka kwa kitovu cha mtoto wa kiume katika sehemu zake za siri na uwezo wa kuzalisha bali ni imani zinazotokana na tamaduni za zamani.

“Hakuna uhusiano wowote ule kwamba kitovu kikimuangukia mtoto anakosa hisia…enzi za wazee wetu wa zamani ili mama awe makini, walikuwa wanasema hivyo,” amesema Dk Mapunda. 

Wataalamu zaidi wa afya wanaeleza kuwa dhana hiyo imerithishwa vizazi na vizazi hadi wakati huu licha ya kutokuwepo ushahidi wowote wa kisayansi na tiba na kwamba muendelezo wa taarifa hizo potoshi unaweza kuwa na athari za kisaikolojia kwa wahusika. 

Mtaalam mwingine wa afya ya uzazi Dk Emmanuel Masali amesema imani za tamaduni za baadhi ya jamii zimefanya wengi waendelee kuamini dhana hiyo iliyopokelewa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. 

Mapitio zaidi ya utafiti unaohusu masuala ya uzazi na watoto yanaonyesha hakuna utafiti wowote uliowahi kufanywa na watafiti wa tiba na sayansi unaohusiana na moja kwa moja athari za kitovu kudondokea kwenye uume wa mtoto na kuathiri uwezo wa kuzalisha. 

Utafiti uliopo unazungumzia tu athari za kutofuata taratibu za kiafya kutunza kitovu cha mtoto ikiwemo uvimbe kwenye kitovu na kuleta kidonda lakini kati ya athari hizo hakuna hata moja inayogusia kushindwa kuzalisha.  

Uamuzi wa NuktaFakti

Dhana hiyo inayosemwa mara kwa mara ikiwemo mitandaoni ni potoshi kwa kuwa hakuna uhusiano wowote wa kitovu kudondokea kwenye uume wa mtoto na uwezo wake wa kuzalisha siku za baadaye. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks