Pepo ya Tanzania ya kumvalisha pete mchumba wako

January 20, 2020 6:55 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni hifadhi ya Taifa ya Ibanda yenye ukubwa wa kilometa za mraba 200.
  • Imesheheni swala na ndege mbalimbali wasiopatikana maeneo mengine duniani.
  • Ni hifadhi ya Taifa inayounganisha mipaka ya Tanzania, Uganda na Rwanda.

Dar es Salaam. Kagera. Unaweza kuwa umewaoona swala wengi katika matembezi yako mbugani. Huenda swala hao uliowaona siyo wale aina ya”Thomson” utakaowaona kwenye pepo hii ya Tanzania ambayo imezinduliwa mwaka 2019.

Ni katika hifadhi ya Taifa ya Ibanda yenye ukubwa wa kilomita za mraba 200 iliyopo kanda ya ziwa, iliyosheheni vivutio vingi kwa ajili ya shughuli za utalii. 

Hata masikio yako yanaweza kuwa yamesikia miluzi na nyimbo nyingi za ndege lakini ni hakika mlio na uzuri wa ndege utakaowaona kwenye hifadhi hii watakaokupatia kitu cha kipekee kupumzisha akili yako.

Huenda umewahi kwenda wakati hifadhi hii ikiwa ni pori la akiba lakini hakika hauwezi kupishana na fursa ya kuitembelea tena kwa sababu itakufanya uwe katika nchi tatu kwa wakati mmoja.

Ndio, hifadhi ya Taifa ya Ibanda iliyopo Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ni hifadhi pekee inayounganisha ardhi ya Tanzania, Uganda na Rwanda huku ikikupatia muonekano thabiti wa mawio na machweo ya anga ya Afrika Mashariki. 


Zinazohusiana


Mambo ya kufanya ukiwa Ibanda

Ukiwa Ibanda, unaweza kufurahia kuwinda wanyama kwenye majani yenye urefu wa hadi mita 1.5 huku viboko, nyani na maua yatakayokufanya ufumbe macho kufurahia hewa iliyojaa harufu nzuri na swala wakubwa aina ya “waterbuck”. 

Usiache kubeba darubini, kofia na miwani ili kujikinga na jua, vumbi na wadudu ili kuendelea kufurahia muda wako kwenye pepo hii yenye eneo maalum kwa ajili ya uwindaji wanyama.

Kufika kwenye hifadhi hii ni rahisi kwa usafiri wa basi, meli na hata wa ndege ukiwa unatokea Bukoba au Mwanza. Kisha utaenda moja kwa moja hadi Kyerwa.

Unataka kumvalisha mpenzi wako pete ya uchumba bila hofu ya kukataliwa? Hifadhi hii ambayo utaifaidi endapo unafurahia vipindi vya mvua, basi muda mzuri wa kutembelea ni Januari hadi Aprili.

Pia, kama unafurahia ukame, Ibanda itakua hifadhi nzuri kwako kuanzia mwezi Juni hadi Septemba. Ikiwa mwaka huu una mpango wa kutembelea mbuga za wanyama, ifanye Ibanda kuwa kipaumbele chako. 

Enable Notifications OK No thanks