‘Panga’ la Rais Magufuli lampitia mkuu wa mkoa wa Morogoro

September 20, 2019 3:02 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amfuta kazi siku chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara mkoani humo.
  • Amemteua Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Loota Sanare kuwa Mkuu wa Mkoa huo. 
  • Ameteua mabalozi watakaokwenda kuwakilisha nchi katika vituo 12 akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Modestus Kipilimba.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Lootha Sanare kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akichukua nafasi ya Dk Steven Kebwe ambaye uteuzi wake umetenguliwa, ikiwa ni muendelezo wa panga pangua kuboresha ufanisi katika utumishi wa umma.

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa leo (Septemba 20, 2019) na  Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi John Kijazi, Rais Magufuli pia amemteua aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Modestus Kipilimba kuwa balozi ikiwa ni juma moja ya kumng’oa katika nafasi hiyo.

Dk Kijazi amesema Rais Magufuli amemteua Musa Masele ambaye alikuwa msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, kuwa mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.

Ikumbukwe kuwa Septemba 17 mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Mnyeti kwa sababu ya kuwepo kwa mgongano wa utendaji wa wawili hao.

Utenguzi huo wa Dk Kebwe na viongozi wengine wa mkoa wa Morogoro umekuja baada ya ziara ya siku tano ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoibua kasoro mbalimbali katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo. 

Mbali na teuzi hizo, pia Rais amefanya mabadiliko mengine ambapo Mkuu wa Wilaya ya Tarime Charles Kabeho, amehamishiwa wilaya ya Chato na Mkuu wa Wilaya ya Chato Msafiri Mtemi amehamishiwa Wilaya ya Tarime.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kuweka jiwe la msingi la kituo cha afya cha Malolo, wilayani Kilosa Morogoro, Septemba 17.2019 ambapo hakuridhishwa na utendaji wa viongozi wa mkoa huo.  Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Uteuzi wa mabalozi 

Pia Rais amewateua mabalozi watakaokwenda kuwakilisha nchi katika vituo 12 akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana ambao watapangiwa vituo vya kazi baadaye. 

Wengine pamoja na Dk Kipilimba ni aliyekuwa Mkaguzi wa ndani wa Serikali, Mohamed Mtonga; Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Jilli Maleko; na Meja Jenerali mstaafu, Anselm Bahati.  

Utezui huo unatokana na vituo hivyo kuwa wazi, Mabalozi kumaliza muda, kustaafu au kurejeshwa nyumbani ambapo watapangiwa kazi nyingine.

Pangua pangua watendaji wa wizara

Mbali na kuteua mabalozi, Dk Magufuli amefanya mabadiliko katika safu za watendaji katika baadhi ya wizara huku akimteua Dickson Nzunda aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayesimamia Elimu,  kuwa katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu masuala ya Bunge. 

Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha, Marry Maganga amepandishwa cheo na kuwa naibu katibu mkuu Wizara ya Fedha. 

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Anthony Sanga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji huku  Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Ally Possi akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo.

Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Gabriel Pascal Malata ameteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Possi.

Wateule wote hao wataapishwa siku ya Jumapili, Septemba 12 Ikulu majira ya saa tisa kamili mchana, Dk Kijazi ameeleza.


Soma zaidi: 


Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemhamisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nicholas William Mkapa na kumpeleka kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Mathias Bulugulu anakuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Elimu) akichukua nafasi ya Nzunda. 

Katika mabadiliko hayo, aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Alfayo Kidata ameteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo yeye anakwenda kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro kwa sababu nafasi yake imechukuliwa na Mhandisi Sanga huku  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Khatibu Kazungu akiteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW