Panda shuka ya Ummy Mwalimu katika siasa
- Katika uongozi wake aliwahi kusimamia ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vya kisasa kama vile MRI, CT Scan.
- Ateuliwa tena baada ya miezi 22 ya kutenguliwa kwake.
Dar es Salaam. Jina la Ummy Ally Mwalimu limegonga vichwa mbali mbali ya habari ndani ya saa chache zilizopita baada Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa mshauri wake wa masuala ya afya ya uzazi, mama na mtoto.
Uteuzi huo uliofanyika jana Juni 2, 2026 umekuja ikiwa ni imepita takribani miezi 22 tangu awekwe kando katika Baraza la Mawaziri Agosti, 2024.
Lakini swali ni je? uteuzi huu wa Ummy ni ishara ya kumrudisha kwenye ulingo siasa?
Kabla ya kulijibu swali hili tuangazie safari yake katika anga za siasa hadi kuwa Waziri wa Afya, sehemu ambayo kama ungewauliza baadhi ya Watanzania wanaofuatilia sekta hiyo wangeweza kusema ilimfaa sana.
Mwanzo wa safari ya kisiasa
Ummy Mwalimu alianza kujihusisha rasmi na shughuli za kisiasa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2007.Â
Umahiri wake katika masuala ya maendeleo ya jamii, afya na utawala ulimfanya kuteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CCM, katika uchaguzi wa mwaka 2010 na kuitumikia hadi mwaka 2015.
Katika kipindi hicho, pia aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, akihudumu kuanzia Novemba 2010 hadi mwaka 2014.
Baadaye alihamishiwa katika nyadhifa nyingine za unaibu waziri, ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Katiba na Sheria, hatua iliyomjengea uzoefu mpana katika utumishi wa umma.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais wa wakati huo Hayati John Pombe Magufuli alimchagua Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Akiwa Waziri wa Afya, alisimamia mageuzi makubwa katika sekta hiyo ikiwemo kusimamia ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini, jambo lililosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Katika kipindi chake, huduma za afya ya mama na mtoto zilipewa kipaumbele maalumu kupitia kampeni za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga pamoja na ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vya kisasa kama katika hospitali za umma.
Aidha, aliongoza juhudi za kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu na bidhaa za afya kupitia maboresho ya mfumo wa ugavi wa dawa nchini.
Miongoni mwa mafanikio makubwa yanayotajwa katika uongozi wake ni kuongoza maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (AMR) wa mwaka 2017– 2022.Â
Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kuandaa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na tatizo hilo.
Pia alisimamia kampeni za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na madhara ya usugu wa vimelea.
Mbali na sekta ya afya, Ummy Mwalimu amekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake na watoto, kusukuma marekebisho ya sheria ili kuondoa ndoa za utotoni nchini.
Jitihada zake katika maendeleo ya jamii na usawa wa kijinsia zilimjengea sifa kama mmoja wa viongozi wanawake waliokuwa na ushawishi mkubwa katika utungaji wa sera za kijamii.
Kipindi cha Covid-19Â
Mwaka 2020, Tanzania ilikumbwa na janga la COVID-19, kipindi ambacho Ummy Mwalimu alikuwa Waziri wa Afya.Â
Alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kuwasilisha taarifa na hatua za Serikali kuhusu ugonjwa huo.
Hata hivyo, kipindi hicho kilizua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi. Baadhi ya wadau wa afya na wachambuzi walikosoa namna taarifa za maambukizi na takwimu za ugonjwa zilivyokuwa zinawasilishwa kwa umma na mjadala kuhusu upungufu wa vifaa kinga kwa wahudumu wa afya katika baadhi ya maeneo.
Licha ya changamoto hizo, wapo wanaomtaja kuwa mmoja wa viongozi waliobeba jukumu kubwa la kusimamia sekta ya afya katika kipindi kigumu zaidi cha janga hilo.
Mabadiliko ya nyadhifa Serikalini
Desemba 2020, Rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Baada ya kuingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021, Ummy alihamishiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, nafasi aliyohudumu kwa kipindi kifupi kabla ya kurejeshwa tena Wizara ya Afya Januari 2022.
Katika muhula wake wa pili kama Waziri wa Afya mwaka 2022 – 2024, aliendelea kusimamia maboresho ya huduma za afya, kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, pamoja na kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kwa matibabu.
Uwakilishi wake Bungeni
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Ummy Mwalimu alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, hatua iliyompa uhalali wa kisiasa kupitia kura za wananchi baada ya miaka mingi ya uwakilishi kupitia Viti Maalum.
Akiwa mbunge, aliendelea kushiriki mijadala ya maendeleo ya taifa, hususan katika masuala ya afya, utawala wa Serikali za mitaa na ustawi wa jamii.
Mwaka 2024, jina lake lilitajwa katika mijadala ya kisiasa iliyohusishwa na changamoto zilizokuwa zikikabili Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ikiwemo mvutano kati ya mfuko huo na baadhi ya hospitali binafsi.
Hata hivyo, hakukuwa na tamko rasmi la Serikali lililohusisha moja kwa moja mabadiliko ya nafasi yake na changamoto hizo.
Siku chache baada ya sakata hilo Ummy aliondolewa katika nafasi hiyo Agosti 14, 2024 na nafasi yake ikachukuliwa na Jenista Mhagama aliyeaga dunia Desemba 11, 2025.
Uongozi wa kimataifa
Mbali na majukumu yake ya ndani ya nchi, Ummy Mwalimu aliwahi kuwa mjumbe wa bodi ya Global Alliance for Vaccines and Immunization (GAVI) akiwakilisha nchi za Afrika zinazotumia lugha ya Kiingereza.
Uwakilishi huo ulimpa nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya kimataifa kuhusu chanjo na mifumo ya afya duniani.
Safari ya Ummy Mwalimu katika siasa ni simulizi ya kiongozi aliyepitia hatua mbalimbali za utumishi wa umma, kutoka kuwa Mbunge wa Viti Maalum hadi kushika wizara nyeti za Serikali.Â
Mwaka 2025, Ummy Mwalimu alijitokeza kuwania tena ridhaa ya CCM kugombea ubunge wa Jimbo la Tanga Mjini.Â
Hata hivyo, hakufanikiwa kuendelea hadi hatua ya mwisho ya uteuzi wa chama baada ya jina lake kukatwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama.