Ongezeko gharama za uagizaji chakula cha samaki zawaibua wavuvi
- Ni chakula kinachotumiwa na samaki wanaofugwa kwenye vizimba na mabwawa.
- Wafugaji wanatumia hadi Sh88.6 milioni kuagiza.
- Serikali yaanza mchakato kujenga viwanda nchini.
Mwanza. Wafugaji wa samaki mkoani Mwanza wameiomba Serikali kutenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula cha wanyama hao ili kuwapunguza gharama za kuagiza chakula hicho nje ya nchi.
Baadhi ya wafugaji wa samaki wa vizimba wamesema hivi sasa wanalazimika kutumia Dola za Marekani 38,000 (Sh88.6 milioni) kuagiza kontena moja kutoka Dola 28,000 (Sh65.3 milioni) kabla vita ya Ukraine na Urusi haijaanza.
Meck Sadick ni mfugaji wa Samaki wa vizimba wilayani Sengerema amesema iwapo Serikali italeta wawekezaji kwenye eneo la chakula cha samaki itafungua milango mingi kwa watu kuwekeza katika sekta hiyo na hivyo kupunguza uvuvi haramu.
“Ufugaji wa samaki wa vizimba una tija kuliko ufugaji wa aina yoyote, kwanza mfugaji anakuwa na uhakika wa kuvuna kile alichopanda tofauti na kwenda kuweka mtego ziwani,” amesema Sadick.
Awali akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa uwekezaji katika sekta ya uvuvi Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Mifumo ya Taarifa wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mafutah Bunini amesema watalifanyia kazi suala hilo hasa kuvutia wawekezaji kuanzisha viwanda vinavyozalisha chakula za samaki wanaofugwa kwenye vizimba.
Kwa sasa, amesema wanaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuwavutia kuwekeza nchini, jambo litakalosaidia kuwapunguzia gharama wafugaji wa samaki.
Pia hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa samaki wa vizimba ili kupunguza uvuvi haramu na kuongeza ulaji kwa mtu mmoja mmoja.
“Lengo la mkutano huu ni kujadili halihalisi ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi ili iweze kuleta tija,” amesema Bunini
Kwa upande wake Meneja wa TIC Kanda ya Ziwa, Girson Ntimba amesema kupitia mkutano huo wadau watajadili kwa kina fursa zilizopo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuwekeza.
Kwa mujibu wa TIC, tangu mwaka 1997 hadi May 2022, sekta ya uvuvi imeanzisha miradi 165 na kutoa ajira 25,269.
Latest
