Ole Nasha awataka wabunifu kutumia changamoto za Tanzania kama mtaji

March 25, 2019 11:01 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Amewataka wabunifu kutumia fursa ya changamoto zilizopo nchini ili kuibua ubunifu katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo ukuaji wa uchumi wa viwanda. 
  • Amesema Serikali iko tayari kutoa ufadhili ubunifu wowote utakaolenga kutatua changamoto za watanzania na nchi kwa ujumla. 

Dar es salaam. Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka wabunifu kutumia fursa ya changamoto zilizopo nchini ili kuibua ubunifu katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo ukuaji wa uchumi wa viwanda. 

Amesema Serikali iko tayari kutoa ufadhili ubunifu wowote utakaolenga kutatua changamoto za watanzania na nchi kwa ujumla. 

Ole Nasha aliyekuwa akizungumza leo (Machi 25, 2019) jijini Dar es Salaam wakati akizindua Wiki Ya Ubunifu inayofanyika katika Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa suku sita, amesema ubunifu sio suala la elimu bali ni uwezo wa kurahisisha maisha kwa kutumia njia mbadala zinalenga kuboresha hali za watu. 

“Ubunifu sio suala la elimu bali ni mtu yeyote kuangalia namna ya kurahisisha changamoto zinazomkabili. Na ni namna ya kuhusisha watu mbalimbali wenye ubunifu, na serikali itakua tayari kufadhili ubunifu utakaolenga na kuonekana kutatua changamoto tulizonazo nchini,” amesema. 

Amesema ili ubunifu ulete matokeo yaliyokusudiwa ni lazima ukidhi matakwa ya wananchi na kuwa sehemu ya kuleta maendeleo na kuboresha uchumi wa nchi.  

“Buni ili kitu kinunuliwe, sio kwakua umependa. Kwenye mashindano tuliyoyaandaa, kulikua na mtu anajaribu kutengeneza injini ya jeti lakini je, ni hitaji kwa Tanzania? Ingeleta maana zaidi kama kungekua na injini ya trekta,” amesema Ole Nasha.

 

 

Wabunifu na wadau mbalimbali wa teknolojia wakiwa katika ufunguzi wa wiki ya ubunifu jijini Dar es Salaam. Picha| Tulinagwe Malopa.

Akizungumzia Wiki ya Ubunifu, amesema imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa sayansi na teknolojia ambapo amewataka waandaji kuhakikisha wanatafuta eneo la wazi litakalowakutanisha watu wengi zaidi kujionea kazi za ubunifu na kuongeza wigo kwa jamii kufaidika na kazi hizo. 

“Kwanini maonyesho ya ubunifu tumeyaweka ndani, kwanini tusiweke sehemu ya wazi ambayo watu wengi wanaweza kuona?” amehoji Ole Nasha.


Zinazohusiana:


Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu yaliyoandaliwa na Costech kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo likiwemo Shirika la Kuendeleza Ubunifu na Rasilimali Watu (HDIF) yanafanyika kwa siku sita  (Machi 25-30) katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Iringa ambapo pia yanahusisha maonesho mbalimbali ya kazi za ubunifu zinazofanyika hapa nchini.  

Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dr Amos Nungu amesema maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa watu mbalimbali kujifunza na kujionea kazi za ubunifu ambao ni msingi wa ujenzi wa uchumi wa viwanda  

“Tunafanya kwa ajili ya kutambua ubunifu wetu lakini pia kwa jili ya kila mdau kuweza kujifunza vitu vinavyoendelea na kutekelezwa na serikali ya awamu ya tano,” amesema.

Enable Notifications OK No thanks