Nusu ya watoto wanaougua saratani hufariki dunia Afrika
- Mwaka 2020 kulikuwa na wagonjwa wa saratani watoto wapatao 52,000.
- kati yao zaidi ya nusu walifariki dunia.
- Vifo hivyo vilichngiwa na athari za ugonjwa wa Corona.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema watoto wanaougua saratani barani Afrika wako hatarini kupoteza maisha hivi sasa kutokana na kushuka kwa huduma za matibabu za saratani katika kipindi cha janga la Corona au COVID-19.
Mratibu wa programu ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kanda ya Afrika wa WHO, Jean Marie Dangou amesema mwaka 2020 kulikuwa na wagonjwa wa saratani watoto wapatao 52,000 kati yao zaidi ya nusu walifariki dunia .
“Tunakadiria kwamba zaidi ya watoto 28,000 walikufa kwa saratani au kansa katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Hii inavunja moyo sana kwa kuwa saratani ya utotoni inatibika ikibainika mapema na mgonjwa kupatiwa tiba stahiki,” amesema Dangou Agosti 13 mwaka huu wakati akitoa taarifa kuhusu ugonjwa huo.
Amesema ili kuokoa maisha ya watoto zinahitajika juhudi za makusudi za uwekezaji za miundombinu na matibabu ya watu wa bara hilo.
Pia amesisitiza uwekezaji mahususi kwenye kukinga na kutibu kansa ikiwemo kutoa mafunzo ya hali ya juu kwa watoa huduma kwa lengo la kupunguza vifo na idadi ya wagonjwa.
“Kila mtu binafsi anawajibika kuchukua juhudi za makusudi za kujielewesha vyema kuhusu saratani ya watoto na dalili za hatari ili kuweza kuongeza ugunduzi wa mapema na kupatiwa matibabu,” amesema Dkt Dangou.
Sababu za kushuka kwa huduma za matibabu za saratani katika kipindi cha janga la Corona au COVID-19 ni pamoja na uchache wa watoa huduma za afya ambao wengi walijikita kuhudumia wagonjwa wa Corona.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa asilimia 72 ya nchi za Afrika zilikuwa na upungufu wa watoa huduma.
Latest



