Miaka 10 ya saratani Tanzania

February 5, 2022 6:48 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasema visa vya ugonjwa huo vimeongezeka kwa kasi.
  • Sababu kubwa ni mtindo wa maisha ikiwemo ulaji mbaya wa vyakula.
  • Wananchi washauri kupima afya na kubadili mtindo wa maisha.

Dar es Salaam. Katika  kipindi cha miaka 10, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani unaochangangiwa na mtindo wa maisha usiozingatia lishe bora na  kutokufanya mazoezi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema  hiyo ni tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.

“Ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora kama kutokufanya mazoezi (tabia bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake…

“Matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi,” amesema Waziri Ummy.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zinaonyesha kuwepo kwa wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo nchini Tanzania. 

Pia katika kila watu 100,000, watu 76 hugundulika kuwa na ugonjwa  wa saratani.

Waziri Ummy aliyekuwa akizungumza jana katika Siku ya Saratani Duniani amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali imeimarisha huduma za kibingwa katika hospitali sita za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi na tiba kwa kuongeza wataalam, miundombinu pamoja na vifaa tiba.

Waziri Ummy ameweka wazi kuwa saratani ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote watoto, watu wazima, wanawake na wanaume.

“Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya,” amesema.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani yaliyofanyika jana jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Afya.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume, koo, utumbo mkubwa na mdogo na saratani ya mdomo na kinywa.

Wanawake wanaathiriwa zaidi na saratani za mlango ya kizazi, matiti na koo.

Hata hivyo, Tanzania imetunga sheria mbalimbali , miongozo na mikakati ya udhibiti wa vihatarishi ili kuweza kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambapo karibu theluthi moja ya Saratani zinaweza kutibika endapo mgonjwa atabainika mapema.

Daktari  bingwa kitengo cha saratani kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando mkoani Mwanza, Masalu Nestory amesema asilimia 60 ya wagonjwa wa saratani wanaopokelewa katika hospitali hiyo wanakuwa kwenye hatua ya nne ya ugonjwa huo hali ambayo inakuwa ni ngumu kutibika kwa tiba za kawaida.

“Wagonjwa hawa wanaofika kwenye stage hizi tiba zake huwa ni ngumu na asilimia 50 ya wagonjwa hao hupoteza maisha aidha wakiwa wanapatiwa matibabu au wanaporudi kwenye maeneo yao ya kazi,” amesema Dk Nestory.

Amesema wanaendelea kutoa ushauri kwa wananchi kuhakikisha wanafuata kanuni za afya lakini kwenda hospitali mapema mara tu wanapoona dalili za uvimbe ili kuchunguzwa iwapo wana dalili za saratani.


Soma zaidi: 



Hali ilivyo duniani

Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) wanaeleza kuwa kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1.

Kati yao, wagonjwa milioni 9.6 hufariki dunia kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50 ya wagonjwa wote wanaongundulika kuwa na saratani.

Aidha, zaidi ya watu  ya millioni 43.8 wanaishi na saratani duniani. 

Ikiwa hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani linakadiriwa kuongezeka na idadi ya wagonjwa wapya kufikia  milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Nyongeza na Daniel Samson

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...