Njia za kusafisha sikio ni kuliacha “lijisafishe lenyewe”

July 9, 2020 10:22 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Watu hutumia njia mbalimbali kusafisha sikio ikiwemo njiti za kiberiti na pamba za masikio na kuishia kupoteza ufanisi wa usikivu wao.
  • Wataalamu wameshauri kutokutumia vitu vya ncha kali kusafisha sikio kwani inaweza kumsababishia mtu matatizo ya usikivu.
  • Ukihisi una tatizo la sikio nenda hospitali ukapate tiba.

Dar es Salaam. Leo asubuhi nikiwa kwenye daladala kutoka Kariakoo jijini Dar es Salaam kuelekea ofisini, niliketi pembeni ya mama aliyeonekana kuianza asubuhi yake na matatizo.

Mbali na kuwa sura yake aliikunja kiasi cha kuweza kukufukuza usimpatie hata salamu, kila muda alipeleka vidole vyake kwenye sikio lake akijitahidi kukabiliana na nilichohisi ni muwasho kwenye sehemu ya sikio ambayo kidole kisingeweza kufika.

Mama huyo alitafakari sana na muwasho ule ulimpelekea kufungua mkoba wake kutafuta kitu ambacho kingeweza kufikia mfereji wa sikio ambao kitaalamu unaitwa “Ear Canal”.

Ebo, mkono wake ulitoka na ufunguo na baada ya kujaribu kufikia sikio lake hakuridhika. Alichana karatasi kutoka kwenye daftari na kukiviringisha na kukipeleka sikioni na macho yake yalionyesha kuwa amepata ahueni.

“Njia pekee ya kusafisha sikio lako ni kuliacha lijisafishe,” amesema Mtaalamu Olomi. Picha| earandsinusinstitute.

Usafi wa sikio ni kati ya vitendawili vingi vinavyowaacha baadhi ya watu wakipoteza ufanisi wao wa kusikia baada ya kusafisha sikio kwa kuvuka mipaka.

Kati ya watu hao ni Allan Gambo ambaye ni mkazi wa Ununio jijini Dar es Salaam ambaye ana wiki mbili sasa tangu sikio lake la kushoto lipoteze ufanisi wake.

“Nilikuwa najisafisha sikio na pamba. Kwenye harakati hiyo, niliishia kusikia maumivu makali. Nilitamani iwe filamu lakini ilikuwa ni kweli,” Gambo ameieleza Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Baada ya mdau huyo kufikishwa hospitali, aliambiwa kuwa nta ya sikio (ear wax) alikuwa ameisukuma na kufikia ngoma ya sikio. Haikupaswa kuwa hivyo.

“Ninaendelea na dawa lakini niliambiwa nisirudie, nikiona sikio lina uchafu, niende hospitali. Sasa hivi inahitajika mtu anayeniongelesha kupitia sikio la kushoto aongee kwa sauti kubwa ndiyo nimsikie vizuri,” ameeleza Gambo.

Hili limekaaje kitaalamu?

Mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam Dk Hans Olomi amesema kile kinachoitwa uchafu (nta ya sikio) kina kazi ya kuilinda sehemu ya ndani ya sikio dhidi ya uchafu kutoka nje wakiwemo wadudu wadogo wadogo na vumbi.

Nta hiyo hukaa sehemu ya nje ya sikio ambayo endapo ikisukumwa, inaweza kufikia ngoma ya sikio na hivyo kusababisha madhara katika mfumo wa usikivu.


Zinazohusiana


Kutatua changamoto ya usafi, Dk. Olomi amesema sikio la binadamu limeumbwa kwa mifumo ya kujisafisha lenyewe.

“Njia pekee ya kusafisha sikio lako ni kuliacha lijisafishe,” amesema Mtaalamu Olomi.

Zaidi, daktari huyo ameieleza Nukta kuwa, kila mara sikio linapofikiwa na vumbi, nta huinasa vumbi hiyo na baada ya vumbi/ uchafu kufikia kikomo, nta hiyo hukauka na kutengeneza kijiduara ambacho hutolewa nje ya sikio.

“Ikishajaa, inajikausha inakuwa ngumu, inakuwa kama mpira mdogo inatoka yenyewe,” amesema Dk Olomi aliyeshauri sehemu ya sikio inayofaa kusafishwa ni sehemu ya nje tu ambayo inahitaji kitambaa laini na maji.

Akizungumzia hali ya muwasho ambayo inawasababisha watu kama yule mama wa kwenye daladala kujikuna, Dk Olomi amesema hali hiyo husababishwa pale sikio linapokuwa na uchafu ukiwemo vumbi.

Amesema endapo huwezi kuukuna muwasho huo, ni vema ukatembelea hospitali na siyo kujichokonoa na vijiti kwenye sikio.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW