Njia sahihi za kumkosoa bosi wako

October 20, 2021 5:23 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Unashauriwa kuangalia “mood” ya bosi wako kabla ya kuelezea kero yako.
  • Hakikisha unatumia busara kuongea naye.
  • Mikanganyiko ofisini hutokea na ni jambo la kawaida.

Dar es Salaam. Huwa unafanya nini pale mkubwa wako wa kazi anapokuwa amekosea? 

Wapo wanaoyamezea mate makosa na kusonga mbele kwani “bosi hanuniwi na hakosei” na sababu ikiwa ni kutaka kulinda kibarua.

Mbali na hao, wapo wanaofunguka na kusema kuwa “bosi hapa kwa kweli haijakaa sawa” na wengine hushindwa kutumia busara pale wanapoamua kuwa wawazi kwa kujibizana na waajiri wao na hivyo kuonekana kuwa watovu wa nidhamu hata wanapokuwa sahihi.

Moja ya rafiki zangu ambaye ni meneja rasilimali watu ameniambia, “mazingira ya kazi yanaweza kuwa na changamoto mbalimbali, kuna siku ambazo hali huwa shwari lakini zipo siku ambazo unaweza kutamani urudi utotoni ili usifaye kazi.”

Katika siku ambazo mambo siyo mambo, mwanadada huyo aliniambia kuwa, mtu anahitaji kuwa na intelijensia ya hisia (emotional intelligence) kukabiliana na hali hizo kwani ofisini ni sehemu yenye watu wenye haiba, tabia na historia tofauti.

“Ni muhimu kufahamu kuwa kwenye ofisi kuna mnyororo wa madaraka. Pale mkubwa wako anapokukosea, ongea naye kwa heshima. Fahamu kikomo chako na kumbuka kuwa kwa lolote utakalo sema, mwisho wa siku utaripoti kwa bosi wako,” aliniambia rafiki huyo aliyeomba kutokutajwa jina lakini nitamuita Maria.

Endapo bosi wako akikufokea, kukaa kimya siyo udhaifu, ni busara. Picha|IStock.

Unapokuwa na la kusema juu ya bosi wako, ufanye nini? 

Jiulize kama itabadilisha lolote

Bila shaka umefanya kazi na mtu huyo kwa muda na hulka yake unaifahamu. Wapo ambao wanaweza kushaurika na kupokea maoni ya wafanya kazi lakini wapo ambao neno lao ni katiba.

Kabla ya kujibizana na kuiweka rehani kazi yako, kutokana na kosa ambalo amelifanya, unaweza kuchukua muda na kufikiria kama kuna sababu ya kufanya hivyo.

Kama haipo, endelea kuchapa kazi na kama mazingira ya kazi hiyo unayaona siyo sahihi kwako, basi huenda ni kengere ya uamsho wa wewe kuanza kutafuta kazi mahala pengine.

Tovuti ya The Corporate Slacker imeandika, “unatakiwa kuwaza kama matokeo ya mazungumzo na bosi wako yatakuwa na madhara kwenye kazi yako ya sasa na hata za baadaye.”


Weka hoja mezani

Kuna vijimakosa ambavyo unaweza kuviacha vipite na upepo lakini yapo yale ambayo yanahitaji kuzungumzwa. Kwa hayo, unahitaji muda sahihi wa kufanya hivyo na ndipo unapohitaji kusoma hisia mtu alizonazo kwa wakati fulani.

Inashauriwa kutokuitisha mazungumzo ukiwa na hasira au kufanya mazungumzo hayo ikiwa mmetoka kujibizana.

Maria amesema, “Endapo alikufokea, usimfokee, mwacha aongee kwani wengine ndiyo humaliza hasira zao hivyo. Baada ya muda, unaweza kumfuata na kumweleza hisia zako.”

Pia, unapoongea naye, unaweza kumpatia ushahidi wa matukio ya zamani ambayo aliwahi kuyafanya na ukayapuuzia. Hiyo inaweza kukusaidia kuonyesha ya kuwa ni kweli unakerwa na jambo analolifanya.

Tafuta muda mzuri wa kuwasilisha hisia zako, usiwe na hasira, na bosi wako awe kwenye hali nzuri pia. Picha| Video Hive.

Ongea naye kupitia wawakilishi

Katika ofisi, kuna vitengo. Kila kitengo kina mkuu wake na msaidizi wake pia. Pale bosi wako anapokufanyia sivyo, unashauriwa kuanzia na ngazi ya chini kumfikia na siyo kugonga hodi kwenye ofisi yake na kuhitisha kikao kama mtu uliye naye karibu.

Maria ameshauri kuonana na wakuu wa idara na kama ikishindikana, kuongea na mameneja rasilimali watu kwani hayo mambo ni sehemu ya majukumu yake.

Kwa ambao wana mahusiano mazuri na mabosi zao, wanaweza onana nao moja kwa moja na kuongea nao kwa lugha nzuri kwani mtu yeyote ambaye ni mstaarabu na anapoelezewa kosa lake, hukubali kusikiliza na kuelewa na hata kujirekebisha.

Tovuti ya Life Hacker imeandika, unaweza kuanza kwa kumsifia mazuri aliyoyafanya, itamsaidia kumweka kwenye mazingira mazuri ya kukusikiliza na pia kutokuchukulia  mazungumzo yako nayeye kama utovu wa nidhamu.

Itamsaidia kuona kuwa unania njema na siyo kuwa unataka kumpanda kichwani.

 

Jambo la kuondoka nalo

Mara nyingi mikwaruzano kati ya wafanyakazi na waajiriwa hutokea kutokana na mipaka ya kazi kutokuzingatiwa. 

Kama kiongozi, unatakiwa kujua kuwa mfanyakazi ana mchango mkubwa kwenye kazi zako na pia kama mfanyakazi, ni muhimu kufahamu kuwa bosi wako anafanya mambo yaende ili mwisho wa mwezi unapofika, hali zenu ziwe vizuri.

Ni muhimu kuheshimiana na kukosoana kwa staha ili kujenga biashara, kampuni na kila kitu mnachofanya.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW