Jinsi ya kuimarisha afya ya akili kazini

October 10, 2024 6:41 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kuboresha mahusiano kati ya wafanyakazi na kuzungumza na wanasaikolojia.

Arusha. Oktoba 10, kila mwaka dunia huadhimisha siku ya afya ya akili ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa matatizo ya afya ya akili duniani kote na kuhamasisha jitihada za kumaliza tatizo hili.

Kwa mujibu wa asasi ya kiraia ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY) katika kitabu chake cha Maswali Yaulizwayo na Jamii Kuhusu Afya ya Akili na Majibu Yake, afya ya akili inahusu ustawi wa mtu katika ngazi kuu tatu ambazo ni  nafsi na utashi, akili na fikra, mwili na hisia/mihemuko.

Hivyo afya ya akili inahusiana sana na jinsi mtu anavyofikiri, anavyojisikia na anavyotenda kwa maana mtu akifikiri vizuri ni rahisi kujisikia vizuri na kutenda mambo mazuri. 

Aidha, Mtu akiwa na fikra hasi, atajenga hisia hasi na kisha matendo yake yatakuwa hasi pia. 

Mwaka huu siku hiyo inaadhimishwa kwa kauli mbiu isemayo “ni wakati wa kuipa kipaumbele afya ya akili mahali pa kazi” ikisisitiza jukumu muhimu la kushughulikia afya ya akili na ustawi kazini, likinufaisha siyo tu watu binafsi bali pia mashirika na jamii kwa ujumla.

Shirika la Kazi Duniani (ILO) linabainisha kuwa karibu asilimia 60 ya watu wote duniani wanafanya kazi zinazowawezesha kupata kupata kipato na kuendesha maisha yao.

Hata hiyo, Karibu asilimia 15 ya watu wazima wenye uwezo wa kufanya kazi walipata matatizo ya afya ya akili mwaka 2019 kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hali iliyosababisha upotevu wa pesa na muda wa kufanya kazi.

Jacqueline Owen Mwanasaikolojia kutoka Shirika la WAJAMAMA ameiambia Nukta habari kuwa afya ya akili mahali pa kazi ni miongoni mwa masuala muhimu ya kuzingatia kutokana na watu kutumia muda mwingi kazini.

“Kwa kawaida watu hutumia muda mwingi kazini kuliko mahala popote hivyo ni rahisi zaidi kupata matatizo ya afya ya akili ukiwa kazini kuliko mahali pengine popote,” amesema Owen.

Mtaalamu huyo amesema miongoni mwa mambo muhimu  ambayo taasisi au mtu binafsi anapaswa kufanya ili kukabiliana na tatizo la afya ya akili ni kujenga mahusiano mema na wafanyakazi wengine katika maeneo ya kazi.

Kwa mujibu wa Owen mahusiano mema baina ya wafanyakazi yatawasaidia kuzungumza na kupunguza msongo wa mawazo pamoja na kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Mwaka 2019, takribani watu bilioni 1 wakiwemo asilimia 14 ya vijana wote duniani walikuwa wanaishi na tatizo la akili ambapo  mtu mmoja  kati ya 100 hujiua na asilimia 58 ya wanaojiua ni watu wenye umri wa chini ya miaka 50. 

Kuweka mazingira wezeshi kazini

Owen ameshauri wamiliki wa kampuni, taasisi na mashirika kuweka mazingira wezeshi katika maeneo ya kazi ikiwemo maeneo maalum ya tahajudi (meditation) maeneo ya kupumzikia pamoja na utaratibu wa kuwaona wataalamu wa afya ya akili mara kwa mara.

“Jambo lingine la kuzingatia hizi taasisi zinaweza kuamua kufanya ‘partnership’ (ushirika) na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) zinazotoa elimu ya afya ya akili au wakaamua kumualika mtaalamu akawa anazungumza na wafanyakazi angalau mara moja kila baada ya miezi mitatu,” ameongeza Owen.

Kwa upande wake Maphosa Banduka, Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Nukta Africa amesema ni muhimu viongozi wa taasisi na kampuni kuweka utaratibu wa kuzungumza na wafanyakazi mara kwa mara na kuratibu milo ya pamoja na michezo mbalimbali ya kiofisi.

“Wakati mwingine kama watu wa management (uongozi) tunatakiwa tufikike kiurahisi ili kama mtu anashida aweze kusaidiwa kwa haraka pia kuna shughuli za kimichezo ambazo unaweza kuziratibu ofisini mara kadhaa au unaweza kutoka na wafanyakazi ili wabadiliahe mazingira hiyo pia inaweza kusaidia,” amesema Maphosa.

Kutenganisha kazi na maisha binafsi 

Mbali na masuala hayo mfanyakazi anaweza kutumia mbinu ya kutenganisha masuala ya nyumbani na kazini ili kuepuka msongo wa mawazo na kuishi maisha yenye furaha.

“Ni vyema kujitambua kwanza kuwa wewe ni mtu wa aina gani kisha unaweza kutumia mbinu ya kutenganisha mambo mfano kazini boss amekufokea au mambo hayaendi hakikisha hayo yote yanaishia kazini na hauyaepeleki nyumbani na ya nyumbani hupeleki kazini,” ameongeza Owen.

Mambo mengine ya kuzingatia kulinda afya ya akili kwa mujibu wa WHO ni pamoja na kupanga ratiba ya masaa ya kazi inayobadilika (flexible working hours) pamoja na kuweka mwongozo unayoshughulikia unyanyasaji na aina zote za uonevu.

Aidha, Owen amebainisha kuwa  baadhi ya dalili zinaoonesha matatizo ya afya ya akili kazini ni pamoja na msongo wa mawazo, kukosa morali na kazi, kushuka kwa kiwango cha kufanya kazi, kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati pamoja na kukosa uzingativu (focus) katika masaa ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks