Nyimbo 10 bora za Bongo Fleva 2024

December 28, 2024 8:00 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Diamond platnumz ameendelea kutetea taji lake kama simba wa msitu ndani ya tasnia ya muziki wa Bongo Fleva.
  • Marioo ni msanii ambaye amekuwa na msimu bora sana kwa mwaka 2024.

Dar es Salaam. Ikiwa tunakaribia kufika ukingoni mwa mwaka 2024, tasnia ya muziki wa Bongo Fleva na Afrobeat Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa, huku wasanii wakichuana na kutoa nyimbo bora ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani. 

Nukta Habari inakuletea nyimbo 10 bora za wanamuziki wa Tanzania kwa mwaka 2024. uchambuzi na mapendekezo ya nyimbo hizi umetokana na data za mtandao ya Spotify, Audiomack, Boomplay na Youtube. 

10. Dah! – Nandy Ft. Alikiba

Nyimbo ya “Dah!”, ni kigongo kilichoachiwa rasmi Februari 2 mwaka huu ikiwa ni moja ya kazi bora kutoka kwa Nandy ‘The African Princess” akishirikiana na mfalme wa muziki wa Bongo Fleva King Kiba ‘Alikiba’

Nyimbo ya ‘Dah!’ imeweza kujipatia umaarufu mkubwa kwa wapenzi wa muziki wa Bongo Fleva huku video yake ikijizolea zaidi ya watazamaji milioni 19 Youtube mpaka kufikia Disemba 27 mwaka huu. Na kwa upande wa Spotify ikifikisha streams zaidi ya milioni 1 na plays zaidi ya milioni 2.4 kwa upande wa Audiomack.

Nandy pia ana historia ya kutoa nyimbo zenye mafanikio makubwa katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva kama wimbo wa “Ninogeshe”, “Kivuruge” na “Number One” akishirikiana na Joeboy, wimbo uliochangia kupanua jina lake kimataifa.

09. “Sensema” – Rayvany

Wimbo wa “Sensema” wa Rayvanny, ulioachiwa rasmi Juni mwaka huu una miondoko ya amapiano iliyotikisa mwaka huu akimshirikisha mzee mzima Harmonize.

Video ya “Sensema” imevutia zaidi ya watazamaji milioni 9.8 katika mtandao wa YouTube mpaka kufikia Disemba 27, 2024, huku Spotify ikiweka rekodi ya zaidi ya streams 400,000, Audiomack ikifunga hesabu kwa zaidi ya plays milioni 1.4.

Rayvanny ameendelea kufanya vizuri kwa nyimbo zake maarufu kama “Tetema” akishirikiana na Diamond Platnumz, wimbo uliotamba kimataifa. “Kwetu”, uliofungua njia yake kwenye ramani ya muziki.”Number One Remix” na Zuchu, wimbo wa mahaba uliotikisa Afrika Mashariki.

08. “Disconnect” – Harmonize Ft. Marioo

Mei mwaka huu, Harmonize na Marioo walituacha tukisisimka kwa hit yao ya “Disconnect”, wimbo uliojaa mahadhi ya kisasa na miondoko laini ya Afro Bongo. Ngoma hii imepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki.

Video ya “Disconnect” imekusanya zaidi ya watazamaji milioni 8.1 YouTube hadi kufikia Disemba 27, huku Spotify ikijivunia streams zaidi ya milioni 1. Katika jukwaa la audiomack, wimbo huu umefikisha zaidi ya plays milioni 1.7. 

Harmonize na Marioo wanajulikana kwa vibao vingine vilivyotikisa kama “Uno”, “Atarudi”, na “Single Again”, zote zikiwa ni vibao vyenye ujumbe mzito na burudani isiyo na kifani. Bila kusahau “Mi Amor”, “For You”, na “Dear Ex” kutoka kwa Marioo ambazo zimeendelea kumweka kwenye kilele cha chati ya muziki Tanzania.

07. “Kunguru” – Mbosso

Wimbo “Kunguru” kutoka kwa mkali wa kuandika ndani ya lebo ya WCB Mbosso, ulioachiwa rasmi Mei mwaka huu. Wimbo wa ‘Kunguru’ umeleta shangwe katika kumbi za muziki nchini huku ukiwa ni wimbo flani hivi wa uchokozi kwa watu walioachana na ‘Ma Ex’.

Video ya wimbo huu imefikisha zaidi ya watazamaji milioni 4.7 YouTube mpaka kufikia Disemba 27mwaka huu, huku Spotify ikijivunia streams zaidi ya 400,000. Audiomack ikiwa na zaidi ya plays milioni 2.5 ya wasikilizaji.

Kwa nyimbo zake zilizopita, Mbosso ameendelea kung’ara na vibao maarufu kama”Hodari”,”Tamba”, na “Baikoko”, ambao ulitikisa chati za muziki barani Afrika.

“Kunguru” ni ushahidi mwingine wa kwanini Mbosso anabakia kuwa moja ya majina makubwa katika muziki wa Bongo Fleva.

06. “Hakuna Matata” – Marioo

Namba sita ya nyimbo bora ya Bonge Fleva inaenda kwa Marioo. Aprili mwaka huu, Marioo aliachia ngoma kali inayokwenda kwa jina la “Hakuna Matata”. Nyimbo yenye ujumbe wa kufurahia maisha bila hofu wala stress. Wimbo huu, ukiwa na mahadhi ya Afrobeat na Bongo Fleva, umefanikiwa kuchangamsha mashabiki wengi na kuleta hali ya ukaribu wa kihisia kupitia sauti na midundo mikali kutoka kwa Marioo. 

Video ya ‘Hakuna Matata’  imevutia zaidi ya watazamaji milioni 5 Youtube hadi kufikia Disemba 27, 2024, huku Spotify ikiripoti zaidi ya streams milioni 1 na kwenye Audiomack, imekusanya zaidi ya plays milioni 2.9.

Marioo ambaye hivi karibuni ameachia album yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘The Godson’ amewahi kufanya vizuri pia na vibao maarufu kama “Mi Amor”, “For You”, na “Dear Ex”.

Marioo ni moja ya wasanii ambao wamekuwa na msimu bora kwa mwaka 2024 Picha | Wetalksound

05. “Wa Peke Yangu” – Jay Melody

Aprili mwaka huu, Jay Melody aliachia wimbo wake wa “Wa Peke Yangu”, ambao umejikita katika maudhui ya upendo wa kipekee na hisia za kumiliki. Ngoma hii imekuwa moja ya nyimbo zilizoteka hisia za mashabiki kwa haraka, huku ikiwa na mchanganyio wa sauti tamu za Jay Melody na midundo laini inayokonga roho.

Video ya ‘Wa Peke Yangu’ kutoka kwa Jay Melody imevutia zaidi ya watazamaji milioni 5.9 katika mtandao wa YouTube mpaka Disemba 27, 2024 huku Spotify ikiorodhesha zaidi ya streams 600,000 na Audiomack ikiripoti zaidi ya plays milioni 2.9.

Jay Melody pia anajivunia nyimbo nyingine zilizofanya vizuri, kama “Nakupenda”,”Sawa”, na “Huba Huba” ambazo zilitikisa tasnia ya muziki wa Bongo Fleva.

04.”Wivu” – DJ Mushizo

Namba tano imeenda kwa ngoma yenye miondoko ya kisingeli inayobamba mpaka sasa. Wivu ni wimbo ulioimbwa na DJ Mushizo akimshirikisha Jay Combat na Baddest 47 huku akiongezeka Ibraa kwenye remix iliyoachiwa Septemba mwaka huu.

Ukiachilia mbali umaarufu ulioupata wimbo huu katika mtandao wa Tiktok, kigongo cha “Wivu” kimejizolea zaidi ya watazamaji milioni 2.8 katika mtandao wa Youtube mpaka kufikia Disemba 27  mwaka huu huku ikipata zaidi ya streams 60,000 na kujizolea plays zaidi ya 57,000. 

Wimbo wa ‘Wivu’ hauna namba kubwa katika majukwaa mbalimbali mitandaoni lakini umepata mafanikio makubwa kutokana na kusambaa kwake kwa muda mfupi sana. 

Hii sio kazi ya kwanza kwa DJ Mushizo lakini ni ngoma ambayo imebamba na kumpa umaarufu mkubwa na mashabiki kuweza kumtambua. Kwa ufupi wimbo wa ‘Wivu’ umekuwa ni wimbo wa Taifa.

03. “Kautaka” – Jaivah

Kibongo bongo msanii Jaivah amekuwa maarufu kutokana na sauti yake mithiri ya mvumo wa radi ambayo mwezi Mei mwaka huu ilishusha ngoma kali inayoendelea kudunda hadi sasa akimshirikisha JFS Music pamoja na Kingtone SA ya “Kautaka”.

‘Kautaka’ ni ngoma yenye miondoko ya amapiano iyojizolea umaarufu mkubwa katika kumbi za starehe na mtandaoni. Katika mtandao wa Youtube imejizolea zaidi ya watazamaji milioni 1.3 na kujikusanyia zaidi ya streams 800,000 Spotify huku ukiwa na plays zaidi ya 400,000 Audiomack 

Jaivah ameendelea kupanda chati za umaarufu kwa vibao vingine maarufu kama “Chawa”, uliotikisa katika vilabu na mitandao ya kijamii, “Mchumba” pamoja na “Sisi Tumezaliwa Hivi”.

“Kautaka” imethibitisha kuwa Jaivah anaendelea kuleta mapinduzi katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva kwa kujaribu mitindo mipya huku akibaki kuwa wa kipekee. 

02. “Siji” – Zuchu

Chini ya lebo ya WCB, Wimbo wa “Siji” kutoka kwa mwanadada mwenye jina lake mjini, Zuchu, ulioachia rasmi mnamo mwezi Mei mwaka huu, umekuwa moja ya nyimbo zinazopendwa zaidi mwaka huu.

Ukijivunia nafasi ya pili kati ya nyimbo 10 bora za Bongo Flava zilizotamba 2024. Nyimbo hii yenye miondoko ya amapiano akimshirikisha mzee mzima Toss ni kazi ya kipekee inayozungumzia maudhui ya kujikubali, uthabiti wa moyo, na hisia za kukwepa vishawishi vya mapenzi yasiyofaa.

“Siji” imejikusanyia zaidi ya watazamaji milioni 11 Youtube mpaka Disemba 27, 2024, huku ikiwa na zaidi ya streams milioni 2  katika mtandao wa Spotify na ikijikusanyia zaidi ya plays milioni 2 Audiomack.

Ngoma hii imevuta hisia za mashabiki wa rika tofauti kutokana na sauti laini ya Zuchu na mashairi yenye ujumbe wa kina. Pia, video ya “Siji” imepongezwa kwa ubunifu na maudhui yanayowakilisha tamaduni za kiafrika kwa njia ya kisasa.

Zuchu ameendelea kuwa mwamba wa muziki wa Bongo Flava na ameacha alama kupitia nyimbo nyingine zilizotikisa kama “Sukari”, wimbo uliojipenyeza katika anga za kimataifa kwa haraka. “Kwikwi” pamoja na “Jaro”, nazo zimeonesha uwezo wake wa kuchanganya midundo ya asili na Afrobeat.

“Siji” ni zaidi ya wimbo; ni ushuhuda wa kipaji cha Zuchu na dhamira yake ya kuendelea kung’aa kimataifa. 

01. “Komasava” – Diamond Platnumz, Mfalme wa Bongo Flava Anaweka Rekodi ya 2024

Mnamo mwezi Mei mwaka huu mkali wa Afrobeat anayeendelea kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya Afrika, Diamond Platnumz akimshirikisha Chley pamoja na Khalil Harrison kutoka Afrika Kusini aliachia wimbo wake wa “Komasava”, ambao ulipaa moja kwa moja hadi kileleni mwa chati za muziki nchini Tanzania na kimataifa. 

Wimbo huu ni ngoma bora ya mwaka, ukishika nafasi ya kwanza katika orodha ya nyimbo 10  bora za Bongo Flava za 2024. 

“Komasava” ni ngoma inayochanganya Afrobeat na midundo ya Kiswahili, huku ikibeba miondoko ya amapiano kutokea Afrika Kusini ujumbe wa sherehe.

Ukiachilia mbali wimbo huu kuchezwa na wasaniii mbalimbali maarufu duniani kama Jason Derulo ambaye alivutiwa na kufanya nae remix, wimbo wa ‘Komasava’ umeshika chati katika mitandao mbalimbali.

Kwa takwimu, “Komasava” imekusanya zaidi ya watazamaji milioni 34 mpaka kufikia Disemba 27, 2024 huku ikijizolea zaidi ya streams milioni 2 Spotify na kupata plays zaidi ya milioni 4 Audiomack. 

Ngoma hii imesifiwa sana kwa uzalishaji wa kiwango cha juu na video ya kuvutia iliyojaa mandhari ya Kiafrika na maonesho ya kifahari. “Komasava” pia imeongeza uzito wa jina la Diamond kama mfalme wa muziki wa Bongo Fleva, akidumisha nafasi yake kama msanii wa kimataifa.

Diamond Platnumz ameendelea kufurahia mafanikio makubwa kupitia vibao vyake vingine maarufu kama “Jeje”, “Waah” akishirikiana na Koffi Olomide, ulioshinda mashabiki barani Afrika,”Zuwena”, wimbo wa hisia uliojaa maudhui ya kijamii.

“Komasava” ni ushuhuda wa ubunifu na mafanikio makubwa ya Diamond, akibaki kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya muziki barani Afrika.

Komasava kutoka kwa Diamond Platnumz ni moja kati ya ngoma zilizofanya vizuri kwa mwaka 2024 Picha | The East African.

Una nyimbo ambayo unafikiri ingeingia katika 10 bora za nyimbo za 2024. Share na sisi kwenye comment hapo chini.

Enable Notifications OK No thanks