Njia rahisi za kulinda macho yako

July 26, 2024 5:06 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuepuka uvutaji wa sigara na kula mlo kamili.
  • Wataalamu wa afya wabainisha kufanya mazoezi, kuvaa miwani ya jua kunasaidia kulinda macho.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa macho ni moja ya changamoto ya kiafya inayowakumba watu wengi ulimwenguni.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kuwa mwaka 2023 kulikuwa na takribani watu bilioni 2.2 wenye changamoto za uoni, ambapo kati yao watu bilioni 1 matatizo yao yangeweza kuepukika na yanaweza kutibika.

Aidha, kwa mujibu wa Wizara ya Afya Watanzania 620,000 wanakabiliwa na matatizo ya kutoona wakati milioni 1.86 wakiwa na changamoto ya kuona kwa viwango vya kati na juu.

Wakati WHO wakibainisha kuwa magonjwa ya kurithi, umri, athari za mionzi pamoja na kisukari kama miongoni mwa sababu za changamoto ya uoni, wataalamu wa afya wamebaini mtindo wa maisha unaweza kuchangia kuimarisha au kuharibu uoni wa macho.

Makala hii inaangazia mbinu mbalimbali za kulinda uoni kama zilivyopendekezwa na wataalamu wa afya kwa kurejea tovuti za kisayansi pamoja na ripoti za WHO.

Soma zaidi: Vyakula vinavyosaidia kuboresha afya ya macho

Kuvaa miwani ya jua

Kwa mujibu wa Chuo cha Sayansi ya Macho cha Marekani (AAO) jua hutoa mionzi ya (ultraviolet (UV) ambayo inaweza kusababisha athari kwenye uoni.

Chuo hicho kinabainisha kuwa kuvaa miwani maalumu ya jua kunaweza kupunguza hatari ya kupata athari kama kuungua kwa mtoto wa jicho, saratani ya macho pamoja na kukulinda na wadudu wanaoweza kuingia machoni.

Hata hivyo, inashauriwa kupata kwanza msaada wa kitaalamu ili kufahamu aina ya miwani unayopaswa kutumia ili kuepuka kukumbana na athari nyingine.

Inashauriwa kupumzika kwa sekunde 20 kila baada ya dakika 20 za kutizama kitu kwenye skrini. Picha l Praxis42 

Kuepuka kutumia skrini kwa muda mrefu

Umoja wa Wataalamu wa Afya ya Macho kutoka nchini Marekani (AOA) umebainisha kuwa ni hatari kutumia kifaa chenye mwanga kwa muda mrefu kwa kuwa kunaweza kusababisha ukavu macho, maumivu ya shingo, mabega, kutoona vizuri, pamoja na kuumwa kichwa.

AOA imependekeza kutumia sheria ya 20-20-20 ili kuepukana na athari za mionzi ya mwanga kutoka kwenye vifaa vyenye skrini kama simu, kompyuta, kompyuta mpakato pamoja na televisheni au runinga.

Sheria hiyo inamtaka mhusika kupumzika kwa sekunde 20 kila baada ya dakika 20 za kutizama kitu kwenye skrini ambapo anatakiwa angalau kutizama kitu kilicho na umbali wa futi 20 kutoka alipo.

Aidha, wasomaji wa vitabu nao wanashauriwa kutumia sheria hiyo ili kuepukana na athari kama vile myopia (kutoona mbali) pamoja na ukungu.

Soma zaidi: Vyakula vinavyosaidia kuboresha afya ya macho

Kufanya mazoezi ya mwili

Wataalamu wa afya kutoka AAO wanabainisha kuwa kufanya mazoezi mara kwa mara kunaweza kupunguza hatari ya kupata changamoto za uoni wa macho kama vile glaukoma na kisukari cha macho kwa kuwa mazoezi huimarisha mtiririko wa damu mwilini.

Chuo hicho kinasisitiza kutenga angalau dakika 150 kwa wiki kwa ajili ya mazoezi ya aerobiki pamoja na siku mbili za mazoezi ya misuli.

“Unaweza pia kufanya mazoezi maalumu ya macho kama kuzungusha macho kwa muda wa dakika moja pamoja na kufumba macho na kufumbua mara 20, mazoezi yanayosaidia kuimarisha misuli ya macho,” imebainisha tovuti ya CNET.

Kuepuka uvutaji wa sigara

Mamlaka ya Dawa na Chakula ya Marekani (FDA) inabainisha kuwa uvutaji wa sigara unahatarisha maeneo matatu muhimu ya macho ambayo ni retina, lenzi pamoja na macula.

FDA inasisitiza kuwa wavutaji wa sigara wapo hatarini mara mbili zaidi kupata magonjwa ya macho kama athari kwenye mtoto wa jicho, kuwa na ukungu machoni pamoja na glaukoma.

Kula mlo kamili

Vyakula tunavyokula kila siku vinaweza kuboresha afya ya macho wataalamu wa afya wanashauri kula vyakula vyenye virutubisho kama vile ‘lutein, zeaxanthin, omega-3 fatty acids, na vitamini A na E’ kwa kiasi kikubwa vinasaidia kulinda afya ya macho dhidi ya athari zinazohusiana na umri, asili ya kazi au matatizo ya kurithi.

Vyakula vingine vinavyoshauriwa ni pamoja na mboga mboga, matunda, vyakula vyenye asili ya protini, pamoja na viazi vitamu.

Mbinu nyingine zinazopendekezwa ni kuepuka kusugua macho kwa sababu kunaweza kusababisha uharibifu wa macho au maambukizi ya magonjwa ya macho. 

Inashauriwa kuosha macho kwa maji safi pale unapohisi muwasho au kumuona daktari pamoja na kusafisha mikono mara kwa mara ili kuepuka maambukizi ya bakteria wanaoweza kuathiri macho yako. 

Enable Notifications OK No thanks