Nje, ndani bajeti ya Lukuvi mwaka 2020-21

May 11, 2020 4:41 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asilimia 61.8 ya bajeti itatumika katika miradi ya maendeleo.
  • Bajeti ya wizara ya ardhi imeongezeka mara mbili ndani ya mwaka mmoja.
  • Wizara hiyo inakusudia kukusanya Sh200 bilioni katika kipindi hicho.

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limeidhinisha bajeti ya Sh133.5 bilioni kwa ajili ya kugharamia shughuli za wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi  mwaka 2020/2021 huku asilimia 61.8 ya fedha hizo zikipangwa kutumika katika miradi ya maendeleo. 

Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/2021 imeongezeka mara mbili kutoka Sh63.9 bilioni ya mwaka 2019/2020 unaoisha Juni 30, jambo litakalotoa fursa kwa wizara hiyo kutekeleza miradi mingi zaidi ya maendeleo.

Hata hivyo, hadi Aprili 30, 2020, Wizara ilikuwa imepokea Sh40.5 bilioni ya fedha zote za bajeti ya mwaka 2019/2020 sawa na asilimia 63.4 ya bajeti au takriban theluthi mbili ya bajeti hiyo ikiwa imesalia miezi miwili tu kumalizia mwaka wa fedha.

William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika hotuba yake ya makadirio ya bajeti ya wizara ya ardhi iliyowasilishwa leo (Mei 11, 2020)  amelieleza Bunge kuwa kati ya fedha zilizoidhinishwa na Sh86.6 bilioni zitaelekezwa katika shughuli za maendeleo.

Lukuvi amesema kati ya fedha hizo za maendeleo, Sh66.3 bilioni ni mapato ya fedha za washirika wa maendeleo wa nje na zilizobaki zitatoka katika vyanzo vya ndani. 

Kiasi cha fedha kingine kitatumika katika matumizi ya kawaida ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wa  wizara hiyo na taasisi zake.

Tume ya Taifa ya mipango ya matumizi ya ardhi imepangiwa kutumia Sh3.9 bilioni ambapo zitatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo  kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika kanda za maeneo ya kilimo pamoja na maeneo yanayopitiwa na miradi ya kimkakati. 

“Maeneo hayo ni pamoja na maeneo inakotekelezwa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) na maeneo yenye vyanzo vya maji ya mto Rufiji unakotekelezwa mradi wa uzalishaji wa umeme (Mwalimu Nyerere Hydro Electric Dam Project),” amesema Lukuvi katika hotuba hiyo.


Soma zaidi: 


Makusanyo ya 2020/2021

Katika mwaka wa fedha 2020/21, Wizara hiyo inatarajia kukusanya Sh200 bilioni kutokana na kodi ya pango la ardhi, ada na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi. 

Ili kufanikisha makusanyo hayo yaliyokusudiwa miundombinu ya Tehama katika Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri, wizara itaimarishwa kusaidia ukusanyaji wa mapato kwa urahisi.

“Tutaboresha kanzidata ya wamiliki wa ardhi kwa kutumia mfumo unganishi wa kielektroniki utakaosaidia kuhifadhi kumbukumbu za ardhi na kuwasiliana na wamiliki kwa urahisi kupitia mawasiliano ya simu na barua pepe,” amesema Lukuvi.

Amesema watahakiki matumizi ya ardhi iliyomilikishwa yakiwemo maeneo ya taasisi za umma na za kidini ili sehemu ya ardhi inayotumiwa kibiashara itozwe kodi stahiki na kuweka utaratibu wa kutoza kodi ya pango la ardhi kwa mashamba makubwa yanayotumika kibiashara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW