Nigeria yatangaza hali ya dharula kukabiliana na tishio la usalama
- Ni kutokana na matukio ya mauaji, na utekaji yanayoendelea.
Dar es Salaam. Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametangaza hali ya dharura ya kiusalama nchini humo kufuatia kuongezeka kwa matukio ya uvunjifu wa amani, ugaidi na uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Taifa hilo la Magharibi mwa Afrika.
Akihutubia Taifa la Nigeria, Novemba 26, 2025, Tinubu amesema hatua hiyo inalenga kuongeza nguvu za kiulinzi na kuimarisha uwezo wa vyombo vya usalama kukabiliana na wimbi la mashambulizi lililoathiri majimbo kadhaa.
Katika hotuba yake, Tunubu ameidhinisha kuajiriwa kwa maafisa 20,000 wa ziada wa Polisi, ili kuongeza idadi ya askari na kufikia jumla ya askari 50,000 ili wakabilianae na changamoto za kiusalama nchini humo.
“Polisi na jeshi vimepewa mamlaka ya kuajiri askari zaidi ili kukabiliana na changamoto za sasa za kiusalama,” amesema Tinubu.
Utekaji wanafunzi, mauaji ndio sababu
Kutangazwa kwa hali ya dharula ya kiusalama nchini Nigeria, kunakuja mara baada ya kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani ikiwemo utekaji wa wanafunzi, mauaji ya raia vijijini, na mashambulizi ya wanamgambo huku visa vya kuvamiwa kwa shule, makanisa, misikiti na mabasi ya abiria vikiongezeka na kusababisha hofu miongoni mwa wananchi nchini Nigeria hivi karibuni.
Mashambulizi hayo yamekuwa yakifanywa na makundi ya wahalifu ambao wameendelea kutumia mianya ya kiusalama kutekeleza matukio ya utekaji kwa ajili ya kupata fedha za ukombozi huku majimbo ya Kebbi, Kwara, Niger, Zamfara, Borno na Yobe yakiripotiwa kukumbwa matukio hayo zaidi.

Mfululizo wa matukio katika maeneo hayo umesababisha adha mbalimbali kwa wananchi na wakazi wa meneo husika huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikiyumba, shule zikifungwa na wakazi wengine kulazimika kuhama makazi yao.
Aidha, Tinubu ameruhusu kambi za Huduma ya Taifa ya Vijana (NYSC) nchini humo kutumika kama vituo vya mafunzo kwa maafisa wapya, wakati maafisa waliokuwa wakihudumu katika ulinzi wa watu mashuhuri wakiwemo viongozi mbalimbali wa nchi hiyo (VIPs) wakitakiwa kupisha nafasi na kupatiwa mafunzo ya haraka kabla ya kutumwa katika maeneo hatarishi.
Idara ya Ujasusi kutuma kikosi maalum msituni
Katika hatua nyingine, Tinubu ameiagiza Idara ya Ujasusi la nchi hiyo (DSS) kuwapeleka mara moja walinzi wa misitu waliofunzwa kudhibiti magaidi na wahalifu wanaojificha kwenye misitu, akisisitiza kuwa katika misitu hiyo hakutakuwa tena maficho kwa maadui wa taifa hilo.
“Wanigeria wenzangu, huu ni wakati wa dharura ya kitaifa, na tunajibu changamoto hii kwa kuongeza nguvu za ulinzi hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi. Nyakati hizi zinahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu. Kama Wanigeria, sote tunapaswa kushiriki katika kuilinda nchi yetu,” ameasa Tinubu.

Mbali na kutangaza hali ya dharura, Tinubu amewapongeza maafisa wa usalama nchini humo kwa mafanikio ya kuwaokoa wasichana 24 wa shule ya Kebbi na waumini 38 waliotekwa katika Jimbo la Kwara, akiahidi kuongeza jitihada za kuwaokoa wanafunzi waliotekwa katika Shule ya Kikatoliki iliyopo Jimbo la Niger, pamoja na Wanigeria wengine ambao bado wanashikiliwa mateka.
Polisi wa majimbo kuanzishwa
Katika hatua ya kisheria, Tinubu ameliomba Bunge la Nigeria kuanza kupitia sheria zitakazowezesha majimbo kuanzisha polisi wa majimbo, ikiwa yatahitaji kufanya hivyo, na kuzitaka taasisi za elimu na nyumba za ibada katika maeneo hatarishi kuimarisha ulinzi na kushirikiana na vyombo vya usalama.
Hata hivyo, kabla ya nchi hiyo kutangaza hali ya dharura ya kiusalama Rais wa Marekani, Donald Trump alisema kuna mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo yanaendelea nchini humo.
Latest