Jinsi ya kutambua fedha bandia,halali

November 26, 2025 8:16 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kutizama alama kama sura ya Mwalimu Nyerere, alama ya usalama ya utepe pamoja na zile zinazoonekana kwa kutumia mwanga wa zambarau

Dar es Salaam. Je umewahi kukutana na kisa mkasa cha fedha bandia? Changamoto hii huwakumba haswa wafanyabiashara wa huduma au bidhaa hususan ambao hawana uelewa wa kutambua noti hizo.

Wahalifu huenda kwa wafanyabiashara ambapo hufanya malipo kwa fedha bandia, huku wao wakijipatia bidhaa halali na wakati mwingine hupata pesa inayotokana na chenji huku wakiwaachia wafanyabiashara hasara na maumivu.

Takwimu za matukio ya uhalifu za mwaka 2024 zimebainisha kulikuwa na makosa 139 ya noti bandia ambayo yameongezeka kidogo kutoka 105 yaliyoripotiwa mwaka 2023.

Licha ya kushamiri kwa makosa hayo, Sheria ya Tanzania imeanisha adhabu kali kwa watakaogundulika kughushi noti bandia ikiwemo kifungo cha maisha.

Ili kukabiliana na uhalifu huo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  imeendesha semina ya kuwanoa wanahabari wa uchumi na fedha juu ya namna ya kutambua noti hallai za Fedha ya Tanzania ili kuongeza uelewa kwa wananchi jambo litakalosaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye noti

Kwa mujibu wa Afisa mwandamizi wa BoT, Dodoma Atufigwege Mwakabalula jambo la kwanza la kuzingatia ili kutambua noti halali ni alama iliyofichika kwenye noti inayoonesha sura ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na thamani ya noti husika (watermark).

Kwa mujibu wa Mwakabalula alama hiyo ya Nyerere kwenye noti halali huonekana kwa uang’avu unapoiweka sehemu yenye mwanga huku kwenye noti bandia huonekana kama imechorwa na baadhi ya noti bandia huwa hazina kabisa.

Jambo lingine la kuzingatia ni alama za vipande vipande zenye kuonesha thamani ya noti inapomulikwa kwenye mwanga ambapo tarakimu kamili za thamani ya noti hutokea, alama hizo huwa hazionekani kwenye noti bandia.

Alama ya usalama 

Noti halali ya Tanzania ina alama ya usalama (security thread) iliyoboreshwa kwenye utepe mwembamba inayoonesha kutembea na kubadilika kwa rangi kwa noti za 10,000 5,000 na 2,000.

Rangi za utepe huo zinaonesha upinde wa mistari mithili ya mawimbi yanayotembea kutoka kushoto kwenda kulia na kinyume chake pale noti hiyo inapogeuzwa geuzwa upande au juu na chini.

Rangi za utepe huo zinabadilika toka rangi ya pinki kwenda kijani kwa noti ya Sh10,000 kutoka bluu kwenda zambarau, kwa 5,000 ni kutoka dhahabu kwenda kijani na  kwa 2,000.

 pia, unapoielekeza kwenye mwanga kuna maneno yanayosomeka ‘BOT na thamani ya noti husika kama BOT 10,000 BOT 5,000 au BOT 2.000.

Kivuli kilichofichika

Kwenye noti halali ya fedha kuna alama maalum iliyofichika yenye kuonesha thamani ya noti husika ambayo  huonekana kuwa angavu noti inapogeuzwageuzwa (Latent image).

Aidha, noti halali huwa na alama ya  pembe zinazoparuza na alama maalum zinazotambulisha thamani ya noti kwa kuipapasa kwa wenye ulemavu wa macho. (Tactile corners and distinguishing marks for the visually impaired).

Alama nyingine muhimu ni pamoja na Spark, hii ni alama maalum ambayo twiga anaonekana ndani yake. Alama hii huwa na rangi ya dhahabu ambayo hubadilika kuwa kijani na kurudia tena kuwa ya dhahabu noti inapogeuzwa kwa noti za Sh 10,000,  5,000 na 2,000.

Zingatia pia, (Microtext lines) au  maandishi madogo sana yaliyolala na kutuna yanayoonekana kwa kutumia vifaa maalum vya kukuzia maandishi (lensi).

Alama zinazoonekana kwa mwanga wa zambarau 

Pamoja na alama zinazoonekana kwa macho, noti halali za Tanzania zina alama maalumu zinazoonekana kwenye mwanga wa zambarau pekee, alama hizo ni pamoja na nyuzi nyembamba zenye rangi tatu zilizofichika.

Alama nyingine inayoonekana kwa mwanga wa zambarau ni wino maalum uliofichika ambayo huangaza noti ikimulikwa kwa mwanga wa rangi hiyo kwa noti za 10,000, 5,000 na 2,000.

Aidha, kuna Namna ya noti yenye tarakimu (Serial numbers) ambazo zinazoongezeka ukubwa na kung’aa zinapomulikwa kwa mwanga maalum wa rangi ya zambarau.

Alama ya mwisho ni kiasi cha fedha husika huonekana katikati ya noti husika inapomulikwa na mwanga huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks